Na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limemkamata Elia Mbwambo (45) mkazi wa Ngaramtoni akiwa na jumla ya Kilogramu 187 za madawa ya kulevya aina ya Mirungi ambayo alikuwa anasafirisha kutoka Ngaramtoni wilayani Arumeru kuelekea Arusha mjini.
Akitoa taarifa hiyo leo jioni ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Justine Masejo, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Ngaramtoni muda wa saa 6:30 Mchana akiwa na gari lake aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T.793 CUY.
Mara baada ya gari hilo kufanyiwa upekuzi ilibainika kwamba kulikuwa na viroba vitatu ambapo viroba viwili vilikuwa kwenye buti na kiroba kimoja kikubwa kilikuwa kwenye kiti cha kati.
Aidha Kamanda Masejo amesema kwamba, mtuhumiwa huyo amekuwa akijihusisha na usafirishaji wa biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha.
Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu ili zisaidie kutokomeza uhalifu na kuzidi kuimarisha usalama.