WILAYA ya Simanjiro Mkoani Manyara imepatiwa
tani 473.8 za mahindi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha
maafa,kitakachotolewa kwa wakazi wa wilaya hiyo wanaokabiliwa na njaa baada ya
kukumbwa na ukame msimu uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi kwenye mji mdogo
wa Mirerani,Mkuu wa wilaya hiyo,Brigedia Jenerali Cosmas Kayombo alisema
mahindi hayo yametolewa kwa maeneo yaliyokumbwa na ukame na yatauzwa sh50 kwa
kilo.
Brigedia Jenerali Kayombo alisema,wilaya hiyo
iliomba kupatiwa kiasi cha mahindi tani 3,000 kutokana na wakazi wengi kuwa na
upungufu wa chakula baada ya kukabiliwa na ukame msimu uliopita wa kilimo.
Alisema kutokana na kuongezewa kiasi kidogo
cha mahindi tani 473.8 tofauti na hitaji lao waliloomba,itawabidi chakula hicho
kidogo walichopatiwa wakigawe kwa kuwapa kipaumbele wana kijiji ambao hawakupata
zile tani 988 za awali.
Hata hivyo,mkuu huyo wa wilaya aliagiza
ugawaji huo wa chakula hicho ufanyike kwa uhadilifu na atawachulia hatua kali
za kisheria watakaohusika kufuja au kutumia chakula hicho tofauti na maelekezo
waliyopatiwa.
“Nadhani wote wameelewa maelekezo yangu na
sitarajii kutokea ufujaji wowote kwani si busara wazazi kula chakula cha watoto
hivyo natarajia zoezi la ugawaji litakwenda kama lilivyopangwa,” alisema
Brigedia Kayombo.
Kwa upande wake,Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka
ya mji mdogo wa Mirerani,Hussein Msokoto alisema wao walipatiwa kiasi cha tani 222.5 ambazo
zitagawanywa kwa watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula.
Msokoto alisema mahindi hayo yatatolewa kwa
watu wenye upungufu wa chakula kwa vitongoji vya
Sekondari,Zaire,Kairo,Songambele A,Kazamoyo ,Songambele B,Songambele
Sokoni,Mirerani na kitongoji cha Kilimahewa.
Naye,Mwenyekiti wa kitongoji cha Kairo Wilbert
Nyari alitoa ombi kwa Serikali kuongeza chakula hicho kwani hakijatosheleza kwa
jamii husika,kutokana na kupatiwa kiasi kidogo cha chakula ili hali mahitaji
yao ni makubwa.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia