MBUNGE
wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara,Pauline Gekul (Chadema) amelalamikia mchakato
wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa kitongoji cha Halla B,Kata ya Nangara Wilayani
Babati kuwa ulitawaliwa na mazingira ya rushwa.
Katika
uchaguzi huo uliofanyika jumapili iliyopita,mgombea wa CCM Edward Paschal
alishinda kwa kupata kura 108 dhidi ya mgombea wa Chadema Paulo John aliyepata
kura 92 hivyo kushinda kwa kura 16.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana,Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara (Chadema)
Pauline Gekul alisema hawakubaliani na matokeo hayo kwani vitendo vya rushwa
vilitumika na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
Gekul
alisema siku moja kabla ya uchaguzi huo,mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Werema
Chambiri alinusurika kupigwa na wafurukutwa wa Chadema akituhumiwa kutoa rushwa
ya sh2,000 na sh,1000 kwa wakazi hao.
“Chambiri
aliokolewa na askari polisi wakiongozwa na msaidizi wa mkuu wa upelelezi wa
wilaya ya Babati,afande Mathayo aliyembeba garini akampeleka nyumbani kwake
badala ya kumpeleka kwenye kituo cha polisi,” alisema Gekul.
Hata
hivyo,Chambiri alikanusha vikali kuwa alikuwa anagawa rushwa kwa wapiga kura wa
kitongoji hicho kwani yeye alikuwa amemtembelea rafiki yake ambaye ni kiongozi
wa CCM wa eneo hilo la kitongoji cha Halla B.
“Nikiwa
kwenye nyumba ya rafiki yangu Christopher walikuja vijana wahuni waliokuwa
wanataka kunifanyia fujo na mimi nikapiga simu polisi waliokuja kunichukua na
kunisindikiza hadi nyumbani kwangu,” alisema Chambiri.
Alisema
yeye hakugawa rushwa kwani hagombei nafasi yeyote ile kwenye kitongoji
hicho,hivyo wanaoeneza propaganda hizo wamefilisika kisiasa na pia mgombea wa
CCM Edward Paschal ni mtu anayejiweza kiuchumi.
“Huwezi
kugawa rushwa katika mazingira kama hayo kwanza mimi sigombei chochote na pia
ni mimi ni mkazi wa kata ya Nangara hivyo huku ni kwangu,hao wameishiwa
sera,sasa wanatunga vitu ambavyo havipo,” alisema Chambiri.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia