Wakili maarufu hapa nchini Nyaga Mawala enzi za uhai wake akiwa anatoa mada ya sheria za wanyama pori mara baada ya waandishi kumaliza ziara yao ya kutembelea hifadhi ya Tarangire
Taarifa za kifo cha Mawalla anayemiliki kampuni kadhaa ikiwamo Kampuni ya uwakili ya Mawalla Advocates, kimeshtua wengi akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema taifa limepoteza kijana mwenye maono, akili na mjasiriamali aliyetajirika bila kuiba.
“Nimepokea
kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Nyaga. Licha ya udogo wake
kiumri, lakini alikuwa mshauri wangu kwenye mambo mengi kiuchumi,
kibiashara na kijamii. Nyaga alikuwa kiongozi wa jamii asiye na mipaka
katika huduma tofauti na wafanyabiashara wengi nchini walishirikiana
naye,” alisema Mbowe.
Mawalla
ambaye ni mtoto wa wakili wa kwanza wa kujitegemea nchini, Juma Mawalla
alikuwa jijini Nairobi kwa matibabu ya kupungaza sumu mwilini kutokana
na madhara ya matumizi ya dawa za shinikizo la damu kwa muda mrefu.
Wakati
kifo hicho cha ghafla cha Mawalla kikitokea, Jiji la Arusha pia
linaomboleza kifo kingine cha ghafla cha mfanyabiashara maarufu wa
madini, Henry Nyiti kilichotokea mkoani Morogoro.
Nyiti
ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Interstate yenye makao yake makuu
eneo la Tengeru, wilayani Arumeru alifariki usiku wa kuamkia juzi akiwa
Mahenge alikokwenda kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini na
anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake eneo la Akheri, Arumeru keshokutwa
Jumanne.
Akimzungumzia
wakili Mawalla, Mbowe alisema mchango wake kwa maendeleo ya jamii
hautasahaulika hasa kutokana na kujitolea kuendeleza taaluma ya uwakili
kwa kudhamini tuzo ya wakili kijana kwa kutoa dola 5,000 kila mwaka
kumsomesha mshindi wa tuzo hiyo.
Mbowe
ambaye mwezi uliopita alipokea hati ya kiwanja chenye thamani ya Sh500
milioni iliyotolewa kwa Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF) na wakili
huyo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, alipendekeza
hospitali hiyo iitwe Nyaga Mawalla Memorial Hospital kama njia ya
kumuenzi.
Mbunge wa
Arusha mjini, Godbless Lema ambaye ndiye mwanzilishi wa taasisi ya ArDF,
alimwelezea Mawalla kama kiongozi, tajiri na kijana aliyetumia akili,
nguvu na rasilimali zake akishirikiana na viongozi wote bila kujali
tofauti zao kiitikadi.
“ArDF
tutauenzi na kuuthamini utu uliouonyesha Mawalla kwa kukamilisha ndoto
ya kuwa na hospitali ya kisasa ya mama na watoto ili kuokoa maisha ya
kundi hilo linapoteza maisha kwa kukosa huduma bora na sahihi,” alisema
Lema.
Fred
Lowassa, mtoto wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa alimwelezea
wakili Mawalla kama kijana aliyeonyesha nidhamu tangu akiwa shule na
aliendelea nayo hadi kwenye kazi na shughuli za kiuchumi kiasi cha
kufanikiwa na kutumia utajiri wake kusaidia jamii. “Kifo hiki ni pigo
siyo tu kwa Arusha bali taifa zima la Tanzania.”
Mchango wa
Mawalla kwenye kuendeleza sekta ya elimu, hasa sheria umetukuka ndiyo
maana alijitolea hata kufundisha bila malipo kwenye vyuo vikuu kadhaa
nchini,” alisema Lowassa.
Pamoja na
kujitolea kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo, Mawalla pia alikuwa
mfadhili wa watoto kadhaa wenye mahitaji maalumu ambapo hadi mauti
yanamkuta, alikuwa akisomesha wanafunzi kadhaa katika ngazi mbalimbali
kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.
Nyumbani
kwake anaishi na zaidi ya watoto saba ambao amewachukua kutoka sehemu na
familia mbalimbali nchini anaowalea, kuwahudumia na kuwasomesha kama
watoto wake wa kuwazaa.
Ingawa
haikuweza kujulikana haraka kutokana watu walio karibu naye wote kudaiwa
kuwa jijini Nairobi, mwili wa wakili huyo unatarajiwa kuletwa nchini
kati ya leo na kesho na kupelekwa moja kwa moja katika chumba cha
kuhifadhi maiti cha KCMC, mjini Moshi kusubiri maziko yanayotarajiwa
kufanyika nyumbani kwao Marangu.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia