BREAKING NEWS

Wednesday, March 6, 2013

WAKENYA WAENDELA KUSUBIRI KWA SHAUKU KUBWA MATOKEO YA UCHAGUZI

Wakenya waliangalia kwa wasiwasi kadri matokeo yanavyoanza kutolewa Jumanne (tareh 5 Machi) kwa uchaguzi mkuu wa nchi, wa kwanza kutoka mzozo uliosababisha wimbi la vurugu miaka mitano iliyopita.
  • Marian Ali Sirat, mwenye umri wa miaka 65, akionyesha kidole chake chenye rangi ya bluu baada ya kupiga kura yake katika kituo cha kupiga kura cha Baraza Park huko Wajir. [Bosire Boniface/Sabahi]
    Marian Ali Sirat, mwenye umri wa miaka 65, akionyesha kidole chake chenye rangi ya bluu baada ya kupiga kura yake katika kituo cha kupiga kura cha Baraza Park huko Wajir. [Bosire Boniface/Sabahi]
  • Kundi la wanaume wakiangalia matokeo ya uchaguzi yanayotolewa kwenye televisheni katika baa huko Kisumu, magharibi ya Kenya, kufuatia uchaguzi wa kitaifa wa tarehe 4 Machi. [Till Muellenmeister/AFP]
    Kundi la wanaume wakiangalia matokeo ya uchaguzi yanayotolewa kwenye televisheni katika baa huko Kisumu, magharibi ya Kenya, kufuatia uchaguzi wa kitaifa wa tarehe 4 Machi. [Till Muellenmeister/AFP]
  • Wapiga kura wakiwa kwenye foleni katika shule ya msingi ya Township huko Wajir. Kujitokeza kwa wingi kwa wapiga kura kuliwafanya baadhi ya wapiga kura kusubiri kwa saa sita kupiga kura zao. [Bosire Boniface/Sabahi]
    Wapiga kura wakiwa kwenye foleni katika shule ya msingi ya Township huko Wajir. Kujitokeza kwa wingi kwa wapiga kura kuliwafanya baadhi ya wapiga kura kusubiri kwa saa sita kupiga kura zao. [Bosire Boniface/Sabahi]
  • Afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) akiwa amebeba masanduku ya kupigia kura yaliyofungwa kwenda kuhesabiwa huko Mombasa tarehe 5 Machi. [Ivan Lieman/AFP]
    Afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) akiwa amebeba masanduku ya kupigia kura yaliyofungwa kwenda kuhesabiwa huko Mombasa tarehe 5 Machi. [Ivan Lieman/AFP]
Matokeo ya baadhi ya sehemu kutoka kwenye vituo vya kupigia kura asilimia 37 kati ya 32,000-- vikiwa na kura halali zaidi ya milioni 4.4 zilizohesabiwa kutoka kwa wapiga kura waliosajiliwa milioni 14.3-- yalitumwa kwenye kituo kikuu cha kuhesabia kura huko Nairobi Jumanne mchana.
Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta alikuwa akiongoza katika nafasi ya wagombea urais lakini Waziri Mkuu Raila Odinga alikuwa akimfuatia kwa karibu, matokeo ya mwisho haiwezi kukisiwa kwa sasa.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ahmed Issack Hassan aliwaambia waandishi wa habari kuwa hatarajii matokeo kamili ya urais ya awali hadi angalau Jumatano.
"Ninataka kuwahakikishia wagombea na vyama vya kisiasa, tafadhali msifanye maamuzi ya pupa, jukumu lao ni kugombea kwenye uchaguzi, jukumu letu ni kupangilia," alisema.
Kwa sehemu kubwa, uchaguzi wa Jumatatu ulikuwa wa amani kwani mamilioni ya wapiga kura walijitokeza kuchagua rais anayefutia, magavana, maseneta, wabunge,wawakilishi wa jimbo wa akina mama na wawakilishi wa kata.
Saa kadhaa kabla ya vituo vya kupiga kura kufunguliwa, mapigano ya umwagaji damu yaliibuka huko Mombasa ambapo askari polisi sita na washambuliaji sita waliuawa, pamoja na mabomu kadhaa ambayo yalimjeruhi mtu mmoja huko Mandera, mji ulio kaskazini mashariki unaopakana na Somalia.

Wapiga kura wakabiliana na foleni ndefu, uandikishaji wa kutumia mkono

Wapiga kura wa Nairobi na vitongoji vyake walikabiliana na siku ngumu wakichomwa na jua kusubiri foleni ndefu kwa saa kadhaa kwa ajili ya fursa kupanga mustakabali wa kisiasa wa nchi.
Ingawa upigaji kura uliendeshwa bila ya matatizo katika maeneo mengi, wapiga kura waliozungumza na Sabahi walieleza kukatishwa tamaa na matatizo ya kiufundi na usimamizi mbaya wa foleni katika vituo vingine vya kupigia kura.
Katika kituo cha kupigia kura katika makazi ya Ongata Rongai katika vitongoji vya Nairobi, Millicent Mutai, mwalimu mwenye umri wa miaka 53, alisena aliamka saa 10 alfajiri ili awe mmoja wa watakaokuwa wa kwanza wakati kituo cha kupigia kura kitakapofunguliwa rasmi saa 12 kamili asubuhi. Hatimaye alipiga kura yake masaa sita baadaye.
"Sikufurahishwa na jinsi viongozi walivyosimamia foleni," aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba licha ya kusubiri kwa muda mrefu, ari yake haikupungua.
"Nilihamasika kusimama kwenye foleni muda mrefu hivyo kwa sababu ninaipenda nchi yangu na ilibidi nishiriki kuijengea mustakabali wake kwa kupiga kura," alisema. "Kama kuna watu waliomwaga damu kupigania uhuru wa Kenya, itanigharimu nini kusimama saa kadhaa kujenga mustakabali wake?"
John Kamau, mwenye umri wa miaka 30, dereva wa taksi ambaye alipiga kura yake katika Shule ya Msingi ya Moi Avenue katika wilaya kuu ya biashara Nairobi, alisema alifurahia kutumia kifaa cha kibiometriki cha utambuzi wa mpiga kura katika kituo chake cha kupigia kura.
Hata hivyo, alisema alihisi kudanganywa, wakati vifaa vilipokosekana na makarani wa kura walikuwa wanakagua uhalali wa wapiga kura kwa kutumia daftari la kuandika kwa mkono.
"Hii ni aibu kwamba baada ya kutumia mamilioni kuwekeza katika teknolojia hizo ilishindwa kufanya kazi kwa ajili yetu," aliiambia Sabahi. "Nafikiri chombo cha uchaguzi hakikufanya majaribio yanayofaa kabla ya uchaguzi ili kusahihisha vikwazo vya kiufundi kabla ya siku ya uchaguzi."
Hassan, mwenyekiti wa IEBC, alikiri kulikuwa na kushindwa kwa takribani asilimia 70 katika kifaa cha kielektroniki.
Katika utoaji wa taarifa kwa vyombo vya habari uliofanyika Bomas ya Kenya -- kituo cha taifa cha kuhesabia kura -- Hassan aliwahakikishia kwamba uhalali na uwazi wa uchaguzi ulikuwa salama, hata kwa utumiaji wa daftari la kuandika kwa mkono.
Alisema viongozi wa IEBC walizidiwa na idadi kubwa ya wapiga kura, hasa maeneo ya mjini, ikifanya iwe vigumu kwao kusimamia makundi ya watu, ambapo hatimaye foleni zilivurugika na kuwalazimu wapiga kura kusubiri kwa saa nyingi.
Vifaa vya biometriki vilidhamiriwa kuwatambua wapiga kura kwa kuweka alama za vidole vyao ili kuhakikisha kama walikuwa wanastahili kupiga kura, na kuzuia wanaojibadilisha majina au 'wapiga kura wasioonekana', ambao walilaumiwa kwa dosari za uchaguzi uliopita.

Wapigakura waelezea kuamini kwao kwa mchakato wa uchaguzi

Pamoja na kukatishwa tamaa, William Onyango, mwenye umri wa miaka 34 ambaye ni dereva wa basi huko Nairobi, alisema alikuwa na imani na mchakato huo.
"Nilifuata mchakato wa maelekezo, lakini nina uhakika kwamba hakutakuwa na kuharibika kwa kura kama vile udanganyifu wa kuwapigia kura watu wengine," alisema Onyango, ambaye alipiga kura katika shule ya msingi ya Olympic huko Kibera.
"Viongozi wa IEBC walikuwa wazi sana katika michakato yao, na kwa sababu hiyo nina uhakika watatoa matokeo ya kuaminika," aliiambia Sabahi.
Paul Mwangi, mwenye umri wa miaka 23, mwanafunzi wa tiba katika Chuo Kikuu cha Nairobi, aliiambia Sabahi alifurahishwa na utulivu wa Wakenya ingawa kulikuwa na foleni ndefu.
"Mchanganyiko katika vituo vingi vya kupigia kura na matukio ya kukosa majina ya wapiga kura katika madaftari ya wapigakura ilikuwa ni sababu kubwa ya kusababisha usumbufu, lakini nina furaha kwamba wapiga kura wengi waliopata matatizo ya majina yao walikuwa watulivu wakisubiri matatizo yao yatatuliwe," alisema Mwangi, aliyepiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Mugomoini katika maeneo ya Langata huko Nairobi.
Alisema hii ilikuwa ni ishara kwamba Wakenya wamekomaa kisiasa na uchaguzi huo hautaruhusu tena kutokea kwa vurugu.

Subira yavuta heri

Zafara Chanzu, mkaazi wa Mombasa mwenye umri wa miaka 39, alisema vurugu katika mkesha wa uchaguzi haziwezi kupunguza uamuzi wake wa kushiriki siku ya uchaguzi.
"Ni siku ambayo mtaa wangu wa Miritini waliisubiri," aliiambia Sabahi. "Kwa kupiga kura tunaweza kupata viongozi ambao watashughulikia kutokuwepo kwa usalama."
Upigaji kura unatokea mara moja kwa kila baada ya miaka mitano, alisema, na ilikuwa busara kwa zaidi ya saa sita kusubiri katika foleni.
"Nilipanga kuwepo katika kituo cha kupigia kura kabla kituo cha shule ya msingi Miritini hakijafunguliwa saa 12:00 asubuhi, lakini [kwa kuwa nje kulikuwa na giza] nilipanga foleni niliyokuta ni ndefu tayari saa 3:00 asubuhi," alisema.
Subira Zongo, mkaazi wa maeneo ya Kisauni huko Mombasa mwenye umri wa miaka 23, aliiambia Sabahi kwamba baada ya kupika kura alijisikia kuwa ametimiza dhamira.
"Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kushiriki katika uchaguzi wa viongozi," alisema. "Pamoja na kujisikia vizuri, ilikuwa pia ni tamko la dharau kwa wanachama waliojitenga wa Baraza la Mombasa."
Katika kuelekea katika uchaguzi kulikuwa na vipeperushi vilivyokuwa vikiwaonya watu kutoshiriki, hata hivyo Zongo alisema ni kupitia ushiriki katika zoezi la kitaifa ndiyo atajisikia kuwa sehemu ya nchi.

Vurugu hazitazuwia kura

Huko Kaskazini Mashariki ya Kenya, wakaazi walisema walikuwa wamefurahia kushiriki katika uchaguzi ambao unaingia katika mfumo wa serikali ya ugatuzi.
Marian Ali Sirat, mkaazi wa Wajir mwenye umri wa miaka 65, alisema anakwenda kupiga kura ili kuhakikisha kuwa mgombea kutoka ukoo wake mdogo wa Fai ndani ya ukoo mkubwa wa Degodia anachaguliwa kuwa gavana wa wadi.
"Kuna hisia za kujivunia wakati mmoja wa ukoo wako yuko kileleni," aliiambia Sabahi mara tu baada ya kupiga kura katika kituo cha kupiga kura cha Baraza Park.
Wakaazi waljitokeza kwenda kupiga kura huko Mandera, licha ya machafuko ya kikoo wakati wa uchaguzi.
"Zaidi ya watu watano waliuawa huko Rhamu [wiki iliyopita], lakini tumeweka kando tofauti zetu na kwenda kuchagua vongozi," alisema Abdi Siyat Ammey, mkaazi wa Rhamu. "Watu wanapigana kwa uongozi wa kisiasa na ndio wakati wa kuamua nani wanataka wawaongoze."
Ammey, mwenye umri wa miaka 35, aliiambia Sabahi kuwa alisafiri hadi Kenya kutoka Sudan kwa dhamira pekee ya kupiga kura. Alisema alipiga kura yake kiasi cha saa 3 usiku kwa sababu ya kuchelewa na vipaumbele vilivyowekwa kwa watu wenye ulemavu, wanawake, wazee na mama wanaonyonyesha.
"Natumai wagombea wa chaguo langu watashinda kama zawadi kwetu sisi tuliojitolea kwa kusafiri kutoka mbali kuja hapa," alisema.
"Tulivunjwa moyo na mwendo wa polepole wa zoezi zima, lakini ni zoezi ambalo hutokea mara moja kila baada ya miaka mitano kwa hivyo kusubiri katika foleni kunalipa," alisema.
Alisema kuwa viongozi waliochaguliwa wana kazi ya kumaliza migongano ya kikoo ya muda mrefu huko Mandera ili kupata ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii kwa haraka. Katika suala la kitaifa, Ammey alisema viongozi wanapaswa kuzingatia mshikamano wa taifa, haki na usawa.
Huko Garissa, licha ya kuwepo kwa vitisho kutoka kwa al-Shabaab, wakaazi walitembea kuelekea vituo kadhaa vya kura kwa ajili ya kupiga kura.
"Kwa kweli, nilitarajia siku ya vurugu kwa sababu ya mashambulizi endelevu ya kigaidi Garissa," alisema Hussein Abdi Aress, mkaazi wa Lagdera mwenye umri wa miaka 26. "Lakini tunamshukuru Mungu siku ilikwenda kwa amani. Sasa ninatarajia utendaji kazi wa serikali mpya na natumai wataanza vizuri kwa sababu tuko nyuma kimaendeleo."

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates