Na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Siku chache tu baada
ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Usalama Mkoani hapa
kuendesha operesheni ya nguvu ya uteketezaji wa madawa ya kulevya aina ya bangi
iliyopo kwenye baadhi ya mashamba yaliyopo wilayani Arumeru, sasa hali hiyo
imechukua sura mpya baada ya wananchi wa maeneo hayo kuungana na askari wa
jeshi hilo kuteketeza madawa hayo.
Hali hiyo ambayo haijawahi
kutokea, imekuja baada ya viongozi wa jeshi hilo kukaa pamoja na wananchi hao
na kutumia dhana ya ulinzi shirikishi kwa kuwaelimisha wananchi hao juu ya
madhara ya madawa hayo ya kulevya hali ambayo imesaidia kuwahamasisha kuamua
kuingia mashambani kufyeka bangi hiyo.
Baadhi ya wakazi wa
vijiji vya Likamba na Imbibya wilayani humo, walisema kwamba mbali na kauli ya jeshi hilo
kwamba operesheni hiyo itakuwa endelevu
pia wamegundua madhara ya madawa hayo.
“Japokuwa tunafanya
biashara ya madawa hayo kwa kuuza kwa kila gunia kwa Tsh 130,000 hadi 150,000
lakini tunaona biashara hii haina uhuru badala yake inatufanya tuishi kwa hofu
kila wakati na pia tumegundua yana madhara makubwa kwa afya ya binadamu”.
Alisema mkazi mmoja wa kijiji cha Imbibya ambaye hakutaka kutaja Jina lake.
Baada ya kufanikiwa
kukamata kwa madawa hayo jumla ya magunia 143 ambayo yalikuwa yanasafirishwa
kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yetu, jeshi hilo mkoani hapa
limeamua kufanya operesheni endelevu ya kuingia mashambani ambapo rasmi ilianza
tarehe 01.03.2013.
Mwandishi wa habari
hii alihakikishiwa na Kamanda wa polisi wa Mkoa huu Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP) Liberatus Sabas kuwa jeshi lake limewasha “moto” ambao hautazimika juu ya
Operesheni hiyo na litaendelea kufanya hivyo mpaka wahakikishe mashamba yote ya
madawa hayo yanateketezwa na kuwataka wakazi wa maeneo mengine waanze
kuteketeza madawa hayo kama wanavyofanya wenzao wa vijiji vya Likamba na
Imbibya.
Alisema katika
operesheni ya mara ya pili iliyofanyika tarehe 04.03 mwaka huu waligundua
kuwepo kwa mimea ya madawa hayo katika bonde linalotenganisha vijiji hivyo
ambayo waliifyeka na kisha kuichoma moto na kufanya jumla ya hekari 120
kuharibiwa kwa siku hiyo.
Tangu operesheni
hiyo ya kuteketeza madawa hayo ya kulevya aina ya bangi ianze kwa siku mbili
tofauti imeonyesha mafanikio makubwa ambapo mpaka sasa jumla ya mashamba yanayokadiriwa
kuwa na hekari 270 toka vijiji vya Likamba na Imbibya vilivyopo wilayani
Arumeru zimeharibiwa kwa kufyeka na kuteketeza kwa moto.