Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa
Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa
na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1).
Ni vyema tufahamu kuwa chimbuko
la Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma limetokana na maboresho
yanayoendelea katika Utumishi wa Umma nchini.
Ambapo miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na marekebisho ya Sera ya
Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 toleo Na. 2 la mwaka
2008 ambapo katika Vifungu Na. 4.6 na
6.6. vya Sera hiyo ambavyo vimetamka kuwepo kwa chombo maalum cha kushughulikia
mchakato wa masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma.
Kwa mujibu wa Sheria, Sekretarieti
ya Ajira katika Utumishi wa Umma ndio chombo pekee chenye wajibu wa
kutekeleza majukumu yafuatayo:-
i)
Kutafuta wataalam
wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa za wataalam.
ii) Kutangaza nafasi wazi za kazi zinazojitokeza katika
Utumishi wa Umma.
iii) Kuhusisha wataalam maalum ili kushirikiana nao kwa
ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji.
iv) Kuwashauri waajiri kuhusu masuala mbalimbali
yanayohusiana na mchakato wa ajira.
v)
Kuandaa orodha ya
wahitimu wa Vyuo na wataalam weledi kwa madhumuni ya kurahisisha rejea za
ujazaji wa nafasi za ajira katika Utumishi wa Umma.
Aidha, kwa mujibu wa Sera
hiyo, kuwepo kwa chombo hiki kutaziwezesha Mamlaka za Ajira nchini (zikiwemo
zile za Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa) kubaki na majukumu yake
ya msingi (Core functions) ambayo yameainishwa katika uundaji wa Mamlaka hizo
ili kuongeza ufanisi.
Kutokana na maelezo hayo
hapo juu ni vyema wananchi wote
wakafahamu kuwa ni kosa kwa mtu au taasisi yeyote ile kuchukua Matangazo ya
Sekretarieti ya Ajira na kuyafanyia marekebisho au kuandaa matangazo mbalimbali
yanayohusiana na mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma kwa lengo la
kupotosha umma ilihali wakijua wazi kuwa taarifa hizo wanazozichapisha au
wanazoziandika katika mitandao ya kijamii hazijatolewa na Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma.
Tumefikia hatua ya kusema
haya kutokana na baadhi ya taarifa zinazohusu mchakato wa ajira hususani uwepo
wa nafasi za kazi zilizopo katika baadhi ya mitandao ya kijamii ikionyesha kuwa
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira ametoa matangazo hayo.
Moja ya tangazo hilo la kughushi na lenye nia ya kupotosha umma ni
lile lililoko katika anwani hii www.eastafricajobscareer.com
lenye kichwa cha habari kinachosomeka “Tangazo
la Kazi Utumishi Tanzania June 2013” ambalo linaonyesha
“Mwisho wa kupokea
barua za maombi ni tarehe 8 Juni, 2013”.
Katibu
anapenda kuwasisitizia wadau wote wa Sekretarieti ya Ajira wanaotafuta kazi
pindi wanapoona matangazo katika Vyombo mbalimbali vya Habari wajiridhishe kwa
kuthibitisha taarifa hizo kama ni za kweli kwa kutembelea tovuti ya
Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz kwa taarifa
sahihi zihusianazo na ajira katika Utumishi wa Umma.
Sekretarieti
ya ajira haiwajibiki na wala haitawajibika kwa Matangazo ama taarifa zozote zinazohusiana
na mchakato wa ajira katika Utumishi wa
Umma ambazo haijazitoa rasmi.
Imetolewa 18 Machi, 2013 na
Katibu,
Ofisi ya Rais,
Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma
Maktaba Kuu ya
Taifa/Barabara ya Bibi Titi Mohammedi
S. L. P 63100, Dar Es Salaam.
Simu; +255 22 2153517
Nukushi; +255 22
2153518
Barua pepe:
katibu@ajira.go.tz
Tovuti; www.ajira.go.tz
Aidha, kwa maelezo zaidi; wasiliana na
Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini kwa Barua pepe; gcu@ajira.go.tz au
Simu; 255-687624975
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia