Waziri Mkuu Mizengo Pinda (kushoto) akiwa na viongozi wa Mfuko wa
Pensheni wa NSSF na viongozi wa serikali mara baada ya kufungua mkutano
wa tano wa wadau mfuko huo leo jijini Arusha katika ukumbi wa mkutano wa
AICC
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesifu juhudi za mifuko ya hifadhi
ya jamii nchini inayomilikiwa na serikali kwa kazi nzuri iliyofanya ikiwemo ujenzi
wa vyuo vikuu mbalimbali kikiwemo cha Dodoma,Nelson Mandela pamoja na jengo la
Bunge la jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mkuu Pinda alitoa pongezi hizo alipokua akifungua
mkutano wa tano wa wanachama wa mfuko wa jamii wa NSSF unaoendelea mkoani
Arusha na kushirikisha viongozi wa mifuko mingine ya ndani ya nchi na ile ya
nje ya nchi.
Alisema pasipo kuwepo kwa mifuko hiyo mambo mbalimbali ya
maendeleo yakiwemo ya ujenzi huo kamwe yasingefanyika kutokana na ufinyu wa
bajeti ya serikali jambo ambalo lilisababisha serikali kuitumia mifuko hiyo kwa
makubaliano ya kulipa deni litakalotokana na shughuli hizo za maendeleo.
Alisema mbali na mchango huo wa ujenzi wa miundo mbinu pia
mifuko hiyo imeweza kuchangia pato la taifa kwa kiasi cha asilimia 11 tofauti
na sekta zingine ambazo bado zina michango midogo katika pato la taifa mbali na
ile ya utalii na madini.
Pia alisema hadi hivi sasa mifuko hiyo ina mtaji wa kiasi cha
shilingi trilioni tano na milioni miambili na arobaini na mbili mtaji ambao
unampa uhakika wa kuendelea kuwepo kwa mifuko hiyo na kamwe haiwezi kutetereka
kwa namna yoyote hata kutokana na misukosuko mbalimbali inayoonekana.
Aliahidi serikali kurejesha madeni yote yanayodaiwa na mifuko
hiyo kutokana na kazi mbalimbali za maendeleo zilizofanywa nayo ili kuwezesha
mifuko hiyo kuendelea kukua na kutoa michango yake katika ukuaji wa uchumi na
maendeleo ya nchi.
Naye mkurugenzi mkuu wa NSSF Ramadhan Dau alisema mwaka huu
shirika lake limekaa na kutathimini changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii
ya watanzania na kuja na kauli mbiu ya Hifadhi ya jamii na ujasiriamali yenye
mikakati mbalimbali ya kuiondoa jamii dhidi ya changamoto hizo.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa mikopo toka
taasisi mbalimbali za kifedha kutokana na na kukosekana kwa mali za kuweka kama
dhamana ambapo tayari shirika lake limeanza kutoa mikop yenye masharti na riba
naafuu ya kiasi cha shilingi bilioni 55.6 ambapo watu 7000 mpaka sasa
wameshanufaika.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa ujuzi na
nidhamu ya biashara kwa wajasiriamali kutokana na ukosefu wa elimu ambapo
shirika lake tayari limeanza mazungumzo na taasisi za serikali ikiwemo Veta,Sido
na nyinginezo ili kuweza kutoa mafunzo hayo kwa wajasiriamali hao.
Pia alitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa uthubutu
na woga kwa wajasiriamali katika kuanzisha biashara na kujiajiri ambapo katika
mkutano huo wamewaalika watu mbalimbali ambao watatoa ushuhuda wao wa maisha
yao ya kujiajiri kama chachu ya wajasiriamali kujiamini na kutuhubutu kufanya
biashara.
Aliwataja watu waliowaalika kuwa ni pamoja na mfanyabiashara
Patrick Mfugale anayemiliki kampuni za Pickkork,mfanyabiashara Salim Salum Bakhresa
na mfanyabiashara maarufu afrika raia wa Nigeria Alhaj Aliko Dangote.
Pia alitaja mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na shirika lake
hilo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama,ujenzi wa majengo
mbalimbali ya kitega uchumi ambapo pia aliweza kutaja matarajio yao mbalimbali
ikiwemo ujenzi wa hospitali ya Apollo katika mji ya Kigamboni jijini Dar es
salaam.
Pia alitaja mradi mwingine wanaotaraji kuufanya ni ule wa
ujenzi wa kituo cha michezo,ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 1000
utakaochangia katika gridi ya taifa utakaofanyika katika mji wa Kibaha mkoani
Pwani pamoja na ujenzi wa viwanda vya bidhaa zitakazotumia rasilimali
mbalimbali zitokanazo na wanyama na mimea.