POLISI WAPIGA MABOMU MIGODINI

Jeshi la polisi limelazimika, kutumia mabomu ya machozi kuwasambaratisha
Mamia ya wananchi wa kijiji cha Naisinyai, wilayani Simanjiro, Mkoa wa
Manyara  waliofunga malango yote ya kuingia na kutoka katika mgodi wa
Tanzanite One Mirerani.Wananchi hao, walianza kukusanyika  jana kuanzia saa 11 alfajiri wakiwa na
silaha  za jadi na kuzuia wafanyakazi wa kampuni hiyo, kutoka na kuingia
katika mgodi huo, ambao unamilikiwa kwa ubia na kampuni ya serikali ya
Stamico na Sky Associate ltd.


Kutokana na vurugu za wananchi hao viongozi wa serikali mkoa wa Manyara,
wakiongozwa na Katibu tawala wa mkoa, Eliakimu Maswi, Kamanda wa polisi
mkoa, Francis Masawe, mkuu wa wilaya hiyo, Zephania Chaula na mkurugenzi
mtendaji wa wilaya Yefred Myenzi kufika eneo hilo.


Wakizungumza na viongozi hao, wananchi wa kijiji hicho, walilalamikia
uongozi wa kampuni hiyo, kushindwa kutekelea baadhi ya ahadi zake, tangu
ilipochukuwa mgodi huo, ikiwepo ahadi ya kutoa ajira kwa wenyeji,kulipia
ada wanafunzi,kutoa huduma ya maji na kutoa fedha za ujenzi wa kituo cha
polisi na madarasa.


Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai,Taiko Laizer alisema tangu uongozi mpya
wa kampuni hiyo kufika, wameshindwa kutekeleza ahadi zake na wameshindwa
kukutana na serikali ya kijiji kwa zaidi ya miaka miwili sasa.


 Wakijibu tuhuma hizo, wakurugenzi wa Sky Associate, Hussein Gonga na
Faisal Shabhai, walikiri kuwepo mapungufu katika utekelezaji wa ahadi
kadhaa kutokana na hali ya kifedha katika kampuni hiyo,

Gonga alisema walikuwa wakikabiliwa na madeni waliyorithi  zaidi ya Sh 12
bilioni na mamlaka ya kodi ya mapato(TRA) na mfuko wa pensheni wa NSSF na
wamelipa kiasi kikubwa cha madeni hayo.


Hata hivyo, walikubali ndani ya wiki moja kutoa kiasi cha tsh 40 bilion kama
ahadi ya ujenzi wa madarasa, kuajiri watu 20 kutoka Naisinyai na kutoa
ajira za muda 35 na kulipia ada za wanafunzi kiasi cha sh 10 milioni.


“tutaendelea kutekeleza ahadi nyingine kwa wakati ikiwepo, kutoa mchanga
mifuko minane kwa kijiji, kukamilisha ujenzi wa nyumba za polisi na kulipa
madai mengine”alisema


Akizungumza katika kikao hicho, Maswi aliwataka viongozi wa Tanzanite one,
kuimarisha mahusiano mema na vijiji vinavyowazunguka na akawataka  viongozi
wa kampuni hiyo, kuheshimu mikataba na serikali ya kijiji.

Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Chaula aliwataka viongozi wa kampuni hiyo, kukaa
mara kwa mara na viongozi wa kijiji ili kuimarisha mahusiano mema na
kuondoa migogoro isiyo na sababu.


Baada ya makubaliano baina ya viongozi wa serikali na viongozi wa tanzanite
One, wananchi walikubali kutawanyika na kuanza kuimarisha mahusiano na
wawekezaji hao.

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.