EPA KUSABABISHA NCHI KUPOTEZA TRILIONI 2

Wakati wabunge wamemsihi Rais John Mafuguli kutosaini mkataba wa
ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA), imebainika kuwa
Tanzania itapoteza dola milioni 984 sawa na zaidi ya sh2 trilioni kwa mwaka
kutokana na kuingia kwa bidhaa kutoka kwenye nchi hizo ambazo hazitalipiwa
kodi.Mhadhiri wa sayansi ya siasa na utawala wa umma wa chuo kikuu cha Dar es
salaam Sabatho Nyamsenda aliyasema hayo juzi mjini Babati mkoani Manyara
kwenye mkutano wa tisa wa mtandao wa wakulima nchini (Mviwata).Nyamsenda alisema athari ya kupoteza mapato hayo kwa Taifa ni kubwa na
awali, Rais Magufuli alishaonyesha njia kwa kukataa kutia saini makubaliano
hayo na pia wabunge walipoukataa imekuwa jambo jema mno.Alisema takwimu zilizotolewa kuwa nchi itapoteza dola milioni 32 sawa na
sh32 bilioni kwa mwaka siyo sahihi kwani ni takwimu za miaka iliyopita ila
kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na taasisi ya South Centre
inaonyesha kuwa nchi itapoteza sh2 trilioni.Alisema taarisi ya South Centre ilianzishwa na Baba wa Taifa hayati
Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kupigania ushirikiano wa nchi za kusini
na fedha hizo zitapotezwa kutoka na ushuru wa bidhaa ambazo hazitalipwa
baada ya mkataba wa EPA.Alisema nchi ambazo zilizokuwa zinatozwa mapato nchini hazitatozwa tena na
nchi nyingine zitashindwa kushindana kwenye soko kutokana na bidhaa za
jumuiya ya ulaya ambazo zinazalishwa kwa unafuu na pia hazitalipishwa kodi.“Kutokana na mkataba huo kutakuwa na upotevu mkubwa sana wa mapato na pia
viwanda vya ndani vitakufa kwani havitaweza kushindana kwenye soko na
bidhaa hizo kutoka kwenye nchi za jumuiya ya ulaya,” alisema Nyamsenda.Alisema nchi ikiingia makubaliana hayo, itasalimisha ushuru, ujenzi wa
uchumi wa viwanda na kuendelea kufanya kazi ya utumwa, kwani viongozi wa
nchi za ulaya wanataka tuendelee kuwa wazalishaji wa malighafi kwenye soko
lao.“Tutaendelea kuzalisha mali ghafi za pamba, kahawa na mazao mengine na
kupeleka ulaya kisha wao wanazalisha nguo wanazivaa na kutuletea mitumba na
kuja kutuuzia sisi bila wao kulipia ushuru wa kuingiza bidhaa,” alisema.Alisema nchi haitakuwa na viwanda vya ndani kwani itashindwa kuvilinda na
ukiweza kuvilinda ni kuhakikisha unajiwekea ukomo wa aina ya bidhaa
zinazoingia nchini ila kwa hali hii tutapoteza dhana ya uchumi wa viwanda.“Wakulima, wafugaji na wazalishaji wa chini wataendelea kufanya kazi za
hali ya chini kwa kuendelea kuchuma pamba, kuchunga mifugo na kurudishwa
kwenye hali ya utumwa kupitia makubaliano ya Epa,” alisema Nyamsenda.Mratibu wa Mviwata wa mkoa wa Manyara, Martin Pius aliipongeza serikali
kwa kutosaini mkataba huo kwani makubaliano hayo yanagusa maendeleo ya
jumla ya wananchi wa Tanzania hasa wakulima wadogo.“Makubaliano haya ya EPA yakipitishwa itakuwa mwisho mbaya kwa wakulima
wadogo kwa sababu kile kidogo watakachokizalisha itakuwa vigumu kuingizwa
kwenye soko la ulaya kulingana na ubora unaohitajika,” alisema Pius.Alisema wakulima wa ulaya wanapatiwa ruzuku za uzalishaji na masoko
tofauti na wakulima wa Tanzania, hivyo mkataba huo utakuwa unaumiza kwani
bidhaa zao zitakuwa na bei ndogo tofauti na bidhaa za wakulima wa hapa
nchini.Mwenyekiti wa Mviwata mkoani Manyara, Emmanuel Hewas alisema mustakabali
wa mkulima mdogo kiuchumi kupitia mkataba wa EPA utakuwa kitanzini, hivyo
nchi ya Tanzania haipaswi kujiunga kwenye ushirikiano huo.Hewas alisema mkataba huo hauna maslahi kwa nchi kwani watafiti na wasomi
wengi wameupinga na pia aliwapongeza wabunge kwa kutoridhia nchi kujiingiza
kwenye mkataba huo ambao hauna tija kwa Taifa.

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.