SEREKALI INATAKIWA ISAIDIE USTAWI WA UBUNIFU ASILI KUKUZA UTALII


Wakati Tanzania ikitarajia kupata watalii milioni 2 ifikapo mwaka 2017, wawekezaji katika sekta hii muhimu wanakabiliwa na changamoto kadhaa ili kuwavutia watalii.
Changamoto hizo ni vivutio vipya vya utalii, majengo, miundombinu, njia za mawasiliano huduma, malazi, chakula na huduma nyingine zinazoendana na sekta hiyo.
Katika kufikia lengo la serikali la kupata watalii milioni hao kwa mwaka, wawekezaji hususan wajasiriamali wazalendo, wameshauriwa kujenga hoteli nyingi hususan zile za ngazi ya kati na huduma nyingine mtambuka.
Jiji la Arusha ambalo ni kitovu kikuu cha biashara ya utalii nchini, limeshuhudia ongezeko la hoteli, baa, migahawa, maduka ya fedha na bidhaa za utamaduni vikiwemo vinyago na mavazi ya asili.
Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii (TTB) mkoa wa Arusha unakadiriwa kuwa na hoteli za kitalii zaidi ya 50.
Ongezeko hilo la hoteli za kitalii, mbali ya kulenga katika kuwahudumia maelfu ya watalii wanaotembelea hifadhi za ukanda wa Kaskazini ambazo ni pamoja na hifadhi ya taifa ya Arusha, hifadhi ya Ziwa Manyara, hifadhi ya Tarangire, na hifadhi ya Serengeti.
Pia, kwa ukanda wa kaskazini kuna vivutio vikubwa ambavyo ni kati ya maajabu saba ya asili ya Afrika, Ngorongoro Kreta na Mlima Kilimanjaro.
Inakadiriwa watu milioni 1.2 wameajiriwa katika sekta hii ambayo mwaka huu inatarajiwa kuliingizia taifa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 3.7, sawa na shilingi trilioni 8.
Kwa hiyo, ongezeko la miundo mbinu kama hii linaweza kutafsiriwa kuwa ni ongezeko la nafasi zaidi za ajira hali inayokwenda sanjari na kaulimbiu ya maadhisho ya Siku ya Utalii Dunia mwaka huu isemayo “Billion tourists, billion opportunities” yaani Watalii bilioni, fursa bililioni.
Siku hii huadhimishwa Septemba 27 kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya kuhuishwa kwa sheria iliyoanzisha Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN-WTO) mwaka 1970.
Lakini jingine lenye umuhimu wake ni kwamba sehemu hizi ni vituo vya burudani kwa wakazi wa Arusha na mamia ya wageni wanaotembelea jiji hili wakiwemo wafanyabiashara, wajumbe wa mikutano na watalii.
Kutokana na mahitaji mapya katika soko la utalii, sasa ubunifu mpya unahitajika hasa kutokana na watalii kupenda sana mambo ya asili, kama majengo, vyakula na huduma mbalimbali.
Mfano, Semu Elias Mbise ambaye amewekeza kwenye mgahawa mpya wa Asili Resort ulioko katikati ya jiji la Arusha anaamini ubunifu pekee ndio utasaidia kukuza sekta ya utalii.
Anasema kikwazo anachokabiliana nacho ni mlolongo wa tozo ambazo zinafanya gharama za uendeshaji kuwa za juu na haoni kama kuna sababu hiyo.
Tozo hizo ni kama vile mrahaba unaotozwa na Shirikisho la Hatimiliki za Wasanii (COSOTA), kutokana na nyimbo au kazi za sanaa zinazorushwa katika vituo vya televisheni na redio.
Tozo nyingine ni ya ukumbi ambayo pia inatozwa na COSOTA na tozo ya vifaa vya kuzimia moto inayotozwa na Wakala wa Zima Moto na Uokoaji. Tozo hizi ni mbali na kodi ya mapato inayotozwa na Mamlaka ya Mapato Wadau wengine wa sekta ya utalii kama vile Nicholaus Minja ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Big Expedition anasema katika msimu wa utalii hutokea watalii kukosa sehemu ya kulala.
Hii inaashiria kwamba bado kuna haja ya uwekezaji wa hoteli za kitalii ili kutoa malazi ya kutosha kwa wageni.
Hatuna haja ya kusubiri wawekezaji wa nje. Ni nafasi na fursa ambayo wawekezaji wa ndani wanaimudu ila Serikali isaidie kuwajengea mazingira mazuri ya kazi.
Watalii wanapokuja nchini na kukosa nafasi ni aibu na inasababisha kujenga sifa mbaya kwa sekta hii muhimu kwa uchumi wa nchi.
Changamoto nyingine ni tatizo la kukosekana ndege za moja kwa moja kutoka mataifa makubwa hadi Tanzania na kuna taarifa kwamba ni kutokana na mifumo ya kodi kutokuwa rafiki.
Hali kama hiyo Serikali inapaswa kuwa makini kama kweli imekusudia kuimarisha sekta hii muhimu kiuchumi.
Wabunifu kama wa migahawa asili wapewe nafasi ya kujiimarisha na siyo kurundikiwa mizigo ya kodi kiasi cha kuwakatisha tamaa.
Serikali kwa kupitia watengeneza sera wake haina budi kubuni mbinu za kutambua namna ya kuweka mazingira ambayo yatachochea wawekezaji wadogo kukuwa.
Kumbuka mfanyabiashara mdogo wa leo ni mkubwa kesho. Kama atadidimizwa leo, ieleweke kuwa hata mapato ya kesho yanaathiriwa.

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.