MSIMU WA TANO WA KAMBI TIBA YA GSM WAFUNGWA ZANZIBAR

 
Na Mwandishi Wetu

Kambi tiba ya GSM Foundation, mpaka jana jioni ilikuwa imefikia mikoa 18 ya Tanzania Bara na mmoja wa Tanzania Visiwani ambapo kwa ujumla wake, imefanikiwa kuwaona watoto zaidi ya 3000 na kuwafanyia oparesheni zaidi ya watoto 250.

Kaimu Mkurugenzi wa taasisi ya Mifupa, Upasuaji na Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili, Dk Othman Kiloloma ambaye pia ndio kuwa Kambi tiba hiyo ya GSM Foundation, amesemahata hivyo wako katika kujipanga na kuona iwapo wanaweza kurudia mikoa ya Rukwa na Pemba ambao kuna uhitaji.

Jana wanakambi wa GSM walimaliza kazi yao visiwani Unguja ambayo kwa mujibu wa Afisa Habari wa GSM Bw Khalfan Kiwamba ilikuwa ni Awamu ya tano ya kambi tiba hiyo na kurudi Dar kufanya tathmini ya kazi iliyofanyika, na kujua jinsi ya kumaliza kabisa tatizola watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Dkt. Yassin Juma kutoka Kitengo cha MOI akiwa katika maandalizi ya kumfanyia upasuaji wa kichwa mmoja ya watoto waliofika Hospitali ya Mnazi mmoja kufanyiwa tiba hiyo. 
Dk Kiloloma alisema kuwa utafiti uliofanywa na Taasisi ya MOI mwaka 2002 unaonyesha zaidi ya watoto 4800 huzaliwa kila mwaka wakiwa na maradhi ya vichwa vikubwa na migongo wazi na kati yao 500 pekee ndiyo wanaoweza kufika hospital na kupatiwa matibabu.

Akizungumzia chimbuko la maradhi hayo Dk Kiloloma alisema kuwa watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi wanaweza kuzaliwa nacho au kupata siku chache baada ya kuzaliwa.

"Kwa wale wanao zaliwa na maradhi hayo ni kwa sababu ya upungufu wa virutubisho ambavyo mama mjamzito anatakiwa avipate kabla ya kushika mimba virutubisho hivo vinapatikana kwenye matunda,mboga za majani,mayai na vyakula vyote vyenye protini, pia maradhi ya mgongo wazi husababisha watoto kupooza na kushindwa kutumia miguu yao,"alisema
Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu ambae pia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya MOI Othman Kiloloma akimueleza Waziri wa Afya Zanzibar (hayupo pichani) jinsi Taasisi hiyo inavyookoa maisha ya watoto wanaokabiliwa na maradhi hayo, (kulia) ni Afisa Habari wa GSM Foundation Khalfani Kiwamba. 
Ofisa habari wa GSM Foundation Khalfani Kiwamba alisema kuwa taasisi yao iliamua kudhamini matibabu ya maradhi ya vichwa vikubwa na migongo wazi baada ya kuelezwa changamoto mbalimbali za matibabu ya maradhi hayo na uongozi wa Taasisi ya MOI.

Joviti Mchuruza akiongea kwa niaba ya wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji aliwashukuru timu nzima ya madaktari hao pamoja na Taasisi ya GSM kwa msaada huo wa matibabu waliowapatia wa watoto wao bure. Aliiomba jamii kuacha kuhusisha maradhi hayo na mila potofu za imani za kishirikina au mikosi kwenye familia hali inayofanya akina mama au baba kutelekezewa watoto.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na ujumbe wa Taasisi ya MOI na GSM Foundation ambao wapo Zanzibar kuwafanyia upasuaji watoto wenye vichwa vikubwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja Mjini Zanzibar. 
Aliwaomba pia wataalam hao wasogeze huduma hiyo karibu na jamii hasa maeneo ya vijijini ambapo wapo watoto wengi wenye maradhi hayo wanateseka na hawana msaada.

"Nawaomba wazazi wenzangu hasa akinamama sababu sisi ndiyo tunakaa na watoto kwa muda mrefu ndiyo tunaoweza kugundua mabadiliko ya mtoto pia tusisikilize maneno ya dhihaka ya watu wa pembeni maradha haya yanatibika kabisa"alisema mzazi huyo

Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo  aliwashukuru madaktari pamoja na shirika la GSM Foundation kwa udhamini huo wa matibabu bure kwa watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi.Pia aliwataka wazazi wenye watoto wenye maradhi hayo wasione aibu kuwapeleka hospitali ili waweze kupatiwa matibabu bure.
Dkt. Mohammed Ali Haji wa Kitengo cha upasuaji vichwa maji na mgongo wazi wa Hospitali ya Mnazimmoja akizungumzia ukubwa wa tatizo hilo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Waziri wa Afya wa Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo wa nne (kulia) akiwa na Dkt. Othman Kiloloma watatu (kulia)wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara na maafisa wa GSM Foundation. 
 


 

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.