LUGOLA :MAWAZIRI ACHENI KUMPOTOSHA RAIS
MBUNGE
wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM) amewaonya baadhi ya mawaziri
kutompotosha Rais John Magufuli kuwa fedha zimepotea, kutokana na baadhi
ya watu kuficha majumbani kwenye magodoro wakati hiyo si
sababu.Sambamba na hilo, amewaonya wabunge wa upinzani, kuacha kuwatumia
vibaya wananchi na kuwachonganisha na Rais wao, baada ya kuona
wamebanwa kulipa kodi.Mbunge huyo alitoa onyo hilo jana wakati
akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka
2017/2018 na Mwongozo wa kuandaa mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka
2017/2018 uliowasilishwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip
Mpango.
“Nyinyi mawaziri ni
abiria na mmekaa siti za mbele kwenye gari analoendesha Rais Magufuli
msimkimbize, baadhi yenu msimpotoshe rais yeye si mchumi mtamletea
matatizo mbeleni, pesa zimepotea si kwa sababu zimefichwa kwenye
magodoro ila zimepotea kwa sababu pesa zote zimewekwa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), zitoeni pesa hizo ziende kwenye mabenki,” alisema.
Alisema Bunge limepoteza
mwelekeo, limekuwa la kulialia na kumlaumu Rais Magufuli kwa sababu
amebana wakwepa kodi na kufafanua “Rais aliliomba Bunge hili limsaidie
kutumbua majibu, tumsaidie mipango ya serikali iweze kutekelezeka ili
kujenga nchi yetu, najua Rais ana nia njema na nchi, Hapa Kazi Tu
inawafanya wafanyabiashara waliozoea kukwepa kodi wamebanwa sasa wanalia
biashara imekufa, watumishi waliozoea posho za hapa na pale, kusafiri
wamebanwa, wabunge tuliozoea kula andazi la inchi 18 sasa tunakula la
sentimita mbili, kwenye kamati tumebanwa posho, tunalialia kisa
tumeshikwa pabaya na kuwaingiza wananchi wanyonge eti hawana pesa.
"Kiongozi wa Upinzani,
Freeman Mbowe umepewa gari na serikali na mafuta unawekewa, yamejaa
kwenye gari, kiyoyozi kipo saa 24 unasema serikali imefilisika huku
unawachonganisha wananchi na Rais wao, unawatumia vibaya wananchi,
Msigwa kama Mchungaji (Peter, Mbunge wa Iringa Mjini) tumia taaluma yako
kuwashauri wenzako wawe kwenye safari hii... Rais Magufuli anatupeleka
Kaanani kuishi maisha mazuri, ametupandisha basi kutupeleka nchi ya
ahadi.
"Nashauri anapoendesha
gari ajue kuna matuta, akiendesha vibaya Watanzania atatuangusha, kuna
zebra na wanafunzi wanavuka, akiona spidi iko 50 apunguze mwendo... na
nyinyi mawaziri mmekaa siti za mbele za gari la Rais, msimpotoshe”,
alifafanua.
Mbunge wa Mtera,
Livingstone Lusinde(CCM) alisema ni lazima uchumi unapokua, uoneshe
kwenye maisha ya wananchi wa vijijini ; na si kuonesha ujuaji wa pointi
kwenye makaratasi.
Alisema “Upinzani
msizunguke kusema serikali imefilisika, semeni ukweli, Mbowe
umefilisika, umeshindwa kulipa madeni, serikali haijafilisika, inalipa
mishahara, inalipa madeni yake”.
Naye Mbunge wa Bunda
Mjini, Esther Bulaya (Chadema) alisema kila sehemu kuna njaa, mtaani
wananchi wanalia hakuna pesa na hata wabunge wamepauka kwa kukosa fedha.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia