Ticker

6/recent/ticker-posts

LEMA AENDELEA KUSOTA RUMANDE

 Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema akiwa amezingira na Askari wakimsindikiza kupanda gari la magereza tayari kwa kurudishwa katika mahabusu ya magereza iliopo jijini Hapa
 Lema aliyevaa nyeusi akiwa anapanda ndani ya gari
Na Woinde Shizza,Arusha
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), jana alishindwa kupata dhamana baada ya mawakili wa Serikali kuwasilisha kwa njia ya mdomo kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ya kupinga uamuzi wa dhamana uliotolewa na Mahakama  ya Hakimu Mkazi Arusha jana.
Mawakili hao walisajili kusudio hilo la kukata rufaa, wakiliwasilisha kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, mbele ya Hakimu Desderi Kamugisha, baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya mawakili hao wa Serikali walioiomba mahakama hiyo isimpe Lema dhamana.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Desderi alisema baada ya kupitia vipengele vya Sheria, huku akirejea maamuzi mbalimbali ya Mahakama Kuu kuhusiana na hoja hiyo, alisema notisi ya kusudio la kukata rufaa inasimama kama rufaa, hivyo inazuia kutekelezeka kwa maamuzi yaliyotolewa katika Mahakama hiyo.
Awali akiwasilisha hoja hiyo ya kusudio la kukata rufaa, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Paul Kadushi, alidai mahakamani hapo kuwa wana kusudio la kukata rufaa na kuwa wameshasajili Mahakama Kuu, hivyo uamuzi wa Lema kupewa dhamana hauwezi kutekelezeka, kwani umeshapingwa Mahakama ya juu.
Kwa upande wao, Mawakili wa Utetezi, wakiongozwa na Wakili Charles Adiel, walidai hawajapata notisi yoyote na kuwa maombi hayo ya kukata rufaa ni sarakasi za kisheria ambayo yamelenga kuzuia utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa mahakamani hapo.
Lema alipandishwa katika Mahakama hiyo Novemba 8, akikabiliwa na kesi mbili za uchochezi, ambapo alishindwa kupata dhamana kufuatia maombi ya mawakili hao wa Serikali ambao walidai kuwa, Lema anakabiliwa na kesi nyingine mbili za uchochezi katika mahakama hiyo, asipewe dhamana kwa kuwa  alipopewa dhamana kwa kesi hizo bado alirudia kufanya makosa kama hayo.
Sababu ya pili ya kuomba mahakama isitoe dhamana hiyo ni kwa ajili ya usalama wa mshitakiwa, huku sababu ya mwisho ikiwa ni kwa ajili ya maslahi ya umma.
Akitoa uamuzi huo kuanzia saa 7:02 mchana hadi saa 8:32 mchana, Hakimu Kamugisha alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili za mahakama hiyo, pingamizi la dhamana halikuwa na sababu za msingi, hivyo mahakama hiyo inatupilia mbali pingamizi hilo na kumpatia mshitakiwa dhamana ambayo masharti yake yatapangwa na mahakama.
Miongoni mwa sababu za kutupilia mbali pingamizi hilo zilikuwa ni kuwa mahakama inatoa dhamana bila upendeleo, kwani ni haki ya mshitakiwa ambayo misingi yake inatajwa katika Ibara mbalimbali katika Katiba ya Nchi, ikiwa ni pamoja na Ibara ya 16(6) b, ibara ya 15 na ibara ya 17.
Aliieleza mahakama hiyo kuwa, hakubaliani na hoja za upande wa mashitaka, kwani zinakosa mashiko katika hoja ya kuwa Lema asipewe dhamana kwa sababu za usalama wake, kwa madai ya kuwa aliyasema maneno hayo ya uchochezi dhidi ya Rais huku akiwa na bastola ambayo anamiliki isivyo halali.
Kufuatia malumbano hayo kuhusiana na notisi ya kusudio la serikali kukata rufaa, kesi hiyo ilikwisha majira ya Saa 10:10 jioni, ambapo ulinzi mkali uliimarishwa katika eneo la Mahakama hiyo, huku baadhi ya wafuasi na viongozi wa Chadema, akiwemo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, wakizuiwa kuingia katika lango kuu la Mahakama hiyo ambapo baadaye waliruhusiwa.
Katika kesi ya kwanza Jinai namba 440, Lema anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi Oktoba 22, Mwaka huu, maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa hadhara, alitoa
maneno yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii.
Wakili Marandu alinukuu maneno yanayodaiwa kusemwa na Lema kuwa: “Rais
Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani, iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu,…. “Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya Katiba, Rais huyo ataingiza taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa
vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”
Katika kesi ya pili ya Jinai namba 441, Lema anakabiliwa na shitaka la uchochezi, ambapo
anadaiwa kutoa matamshi yenye chuki, kuibua nia ovu kwa jamii.
Alidai kuwa Oktoba 23, mwaka huu, katika mkutano wa hadhara viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa, Lema alitoa maneno kuwa; “Kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshachukua maisha yake.”
Aliendelea kudai kwamba, mtuhumiwa huyo alitoa kauli hizo kinyume cha Sheria na kifungu cha 63(B) cha kanuni ya adhabu sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.


Post a Comment

0 Comments