WAZIRI MKUU AWAAKIKISHI WANANCHI UMEME BILA MGAWO


Image result for WAZIRI MKUU
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imedhamiria kusambaza umeme wa uhakika nchi nzima na kuhakikisha hakutakuwa na mgawo wa umeme. Hivyo ametaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kujipanga chini ya waziri wake anayemwamini kuhakikisha hakutakuwa na mgawo wa umeme.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa uboreshaji miundombinu ya umeme ya Jiji la Dar es Salaam jana na kueleza kuwa sasa umeme wa uhakika umepatikana na ni vema wananchi kutumia uwepo huo kwa kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa.
“Niwahakikishie mipango hii iliyopo ya uhakika katika kuwaletea umeme wa uhakika nchi nzima ili kuendesha uchumi wa viwanda liokusudiwa kwa ufanisi,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa uememe wa uhakika baada ya kukamilika jijini Dar es Salaam, utasambazwa katika mikoa mingine kwa kuanzia wakati serikali ikijiandaa kuhamia mkoani Dodoma kutakuwa na mradi kama huo kwa kuanzia na mikoa ya Mwanza, Tanga, Mbeya, Arusha na Dodoma.
Alisema serikali imetenga Sh trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 nchi nzima kwa kupitia Mpango wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ili kila mwanakijiji kutumia umeme katika uzalishaji mali.
Alisema serikali kwa kutambua wananchi wasio na uwezo vijijini imepunguza bei ya kuvuta umeme na kuwa Sh 27,000 tu ikiwa ni jitihada kuboresha miundombinu kufikia malengo ya asilimia 75 ifikapo mwaka 2025.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema mradi huu ulihusisha ujenzi wa kituo kikubwa cha kupozea umeme cha megawati 100, ujenzi wa njia za usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 132 katika maeneo mbalimbali ya jiji kupitia chini ya ardhi. Umejengwa kwa msaada wa Serikali ya Finland.

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.