MKAZI wa kijiji cha Bonga wilaya ya Babati mkoani
Manyara,Ally Saidi (25) ambaye ni mvuvi wa samaki,amefariki dunia baada ya mtumbwi
aliokuwa anavua nao samaki ziwa Babati,kupinduliwa na kiboko,kwenye kijiji cha
Himiti.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho,Kamanda wa polisi
mkoani Manyara Kamishna msaidizi,Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilitokea upande
wa eneo la kijiji cha Himiti,kwenye Ziwa Babati mkoani humo.
Kamanda Sabas alisema chanzo cha kifo cha Saidi,ni mtumbwi
aliokuwa anautumia kuvulia samaki kwenye ziwa hilo,kuvamiwa na kiboko na
kupinduliwa kisha akatumbukia ziwani na kufariki dunia papo hapo.
“Huyo mvuvi pamoja na kufanya shughuli za majini lakini hajui
kuogelea hivyo kiboko huyo alipoupindua mtumbwi wake alizama ziwani akanywa
maji mengi na kufariki dunia kwani kwenye mwili wake hakuna jeraha lolote,”
alisema.
Kamanda huyo alidai kuwa,wakati wa uchunguzi wa tukio
hilo,walikuta alama ya jino la kiboko huyo,baada ya kuung’ata mtumbwi huo na
kuupindua hali iliyosababisha Saidi kutumbukia ziwani na kufariki dunia.
Alisema kuwa,mwili wa marehemu huyo umeshakabidhiwa kwa
ndugu zake kwa ajili ya shughuli za mazishi,mara baada ya kufanyika uchunguzi
wa daktari na jeshi la polisi.
Kamanda Sabas alitoa wito kwa wavuvi wote,wachukue tahadhari
pindi wanapoendesha shughuli zao japokuwa hivi sasa Ziwa Babati limefungwa na
kupigwa marufuku kuendesha uvuvi eneo hilo tangu mwaka jana.