ILI kubaini mapungufu na mafanikio
ya miradi ya kata,Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro
mkoani Manyara wamesomewa taarifa ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kipindi
cha Julai hadi Desemba 2011.
Hali hiyo imetokana na agizo la
mkuu wa mkoa huo,Elaston Mbwilo
alivyoziagiza halmashauri za wilaya za mkoa wa Manyara kufuata utaratibu
huo ili kubaini kata ambayo haikutekeleza miradi yake iliyopangiwa.
Katika utaratibu huo mpya,mlezi
wa kata,Ofisa Tarafa,Diwani na Ofisa Mtendaji wa kata husika husimama mbele ya
Baraza hilo na kuwasomea madiwani,taarifa ya miradi yao ya maendeleo
iliyofanywa kwa kipindi cha miezi mitatu.
Akisoma taarifa ya kata ya
Orkesumet,Ofisa mtendaji wake,Shaaban Mkopi alitaja baadhi ya miradi
iliyokamilika ni ukarabati wa nyumba ya mkuu wa shule,ujenzi wa wodi ya wazazi
kituo cha afya na ukarabati wa mabweni.
Naye,Diwani wa kata ya Msitu wa Tembo,Michael
Sinjori alisema baadhi ya miradi waliyoitekeleza ni ujenzi wa kituo cha
polisi,ujenzi wa nyumba ya mwalimu wa shule ya sekondari na ukarabati wa ofisi
ya kata hiyo.
Hata hivyo,kata mbili za Terrat
na Mirerani hazikusomewa taa
rifa zao,baada ya madiwani wake,Robert Saitabau na
Justin Nyari kudai kuwa taarifa hizo hazikupitiwa na kamati za maendeleo za
kata zao.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kwa afya
ya kikao hiki naomba taarifa ya kata yangu ya Terrat isisomwe,kwani Ofisa
mtendaji wa kata William Wanga hakuishirikisha kamati ya maendeleo ya kata
yetu,” alisema Saitabau.
Kwa upande wake,Nyari alisema
taarifa hiyo isisomwe kwenye Baraza hilo kwani imeandaliwa na Ofisa mtendaji wa
kata yake,Valentine Tesha bila kuishirikisha kamati ya maendeleo ya kata ya
Mirerani (WDC).
Kutokana na hali hiyo,Mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya hiyo,Peter Tendee na wajumbe wa Baraza hilo
walikubaliana na madiwani hao kutosomwa kwa taarifa hizo kutokana na maofisa
hao kutowashirikisha wakati wa uandaaji.
“Nadhani hii ni kutokana na jambo
hili kuwa geni,maofisa watendaji wa kata mnapaswa kukaa pamoja na kamati zenu
za maendeleo na kuandaa kitu kizuri kuliko waheshimiwa madiwani wenu waje
kuziona hapa,” alisema Tendee.