WAANDISHI WAHABARI WAASWA KUTOA ELIMU YA KATIBA MPYA


Mkuu wa mkoa wa Manyara Elaston Mbwilo amewaasa waandishi wa habari kuielemisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua mchakato wa mabadiliko ya kupata katiba mpya ambayo imeelezwa kuwa ni wajibu kwa kila mmoja kufahamu mabadiliko hayo.

Mkuu huyo alitoa rai hiyo wakati alipokuwa   mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa habari na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa waandishi wa habari wana umuhimu mkubwa katika kuielimisha jamii juu ya kile kinachoendelea.

Alisema kuwa waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kutoa elimu hiyo ili kuiwezesha jamii kutambua yale yanayofanywa na serikali katika mchakato huo ambapo mabadiliko hayo yanagusa masuala mbalimbali ya maisha yao ya kila siku.

“Habari ni elimu na ufahamu na vyombo vya habari vina umuhimu wake kwani Serikali imeshindwa kutekeleza majukumu mbalimbali kwa sababu jamii haina habari kwa kile kinachoendelea hawana habari na kiunganishi ni nyinyi”alisema Mkuu huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Mkoani Manyara(MAMEC) Benny Mwaipaja alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili katika kuwafikia wananchi wa maeneo ya vijijini ni ubovu wa miundombinu pamoja na ushirikianano uliopo kati yao na viongozi.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alitoa pongezi kwa umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini UTPC kwa kuwawezesha kuwakutanisha na wadau wa habari na kusema kuwa itawawezesha kufanya kazi za uandishi kwa urahisi kutokana na wadau wengi kuonyesha kutoa ushirikiano.

Mkutano huo ambao uliweza kuzishirikisha taasisi mbalimbali  za kiserikali na zisizo za kiserikali,wabunge,wakurugenzi,wakuu wa wilaya,makampuni,viongozi wa dini na viongozi wa ngazi mbalimbali za serikikali.  

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post