ZAIDI ya watu 56 wa kijiji cha
Shambarai wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara hawana mahali pakuishi baada ya
nyumba zao kubomoka na kuezuliwa mapaa na upepo mkali ulioathiri nyumba 14 na
mazao yaliyokuwa mashambani.
Akizungumza na
waandishi wa habari,Diwani wa kata ya Shambarai,Alais Mbarnot alisema tukio hilo
lilitokea kwenye kijiji hicho, saa 12 jioni ambapo upepo huo mkali
uliosababisha tatizo hilo uliambatana na kimbunga.
Mbarnot alisema nyumba ya mwalimu
wa shule ya msingi Shambarai,Salma Mpinga ni miongoni mwa nyumba zilizopata
madhara ya kubomoka pamoja na miti na mazao ya mihogo,mahindi,maharage na
migomba iliyokuwa shambani.
Hata hivyo,alisema kuwa katika
tukio hilo hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa au kufariki dunia zaidi ya mazao
mengi yaliyokuwa yamestawi mashambani kuathirika na upepo huo mkali
ulioambatana na kimbunga.
Alisema hadi hivi sasa wahanga
hao 56 walioathiriwa na janga hilo wanaishi kwa ndugu,jamaa na majirani wakati
wakisubiri hatua nyingine zitakazofuata kwani nyumba zao kwa muda huu hazifai
kutumika.
Mmoja kati ya shuhuda wa tukio
hilo ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema upepo huo umeathiri sehemu
kubwa ya vyakula vilivyokuwa mashambani na nyumba hizo 14 kubomoka huku
nyingine zikipata nyufa.
“Huo upepo ulikuwa mkali kweli
kweli,kwani tangu nizaliwe sijawahi kuona upepo mkali kama huo,nilishuhudia
miti mikubwa kama migunga yenye mizizi iliyosambaa ardhini ikiangushwa chini na
upepo huo,” alisema.
Alitoa wito kwa Serikali ya
wilaya hiyo au mkoa huo,kujaribu kuwasaidia wahanga hao kwani hawakupenda
kutokewa na hali hiyo ambapo wengi wao wana kipato kidogo hivyo watazidi
kuteseka hadi wajenge nyumba nyingine.