MKUU wa wilaya ya Simanjiro
mkoani Manyara,Khalid Mandia amevitaka vikundi mbalimbali vya ujasiriamali
wilayani humo kuungana ili waweze kujikomboa kupitia mikopo inayotolewa na
taasisi za fedha.
Mandia aliyasema hayo ,wakati
akizundua kikundi cha Jitegemee,kilichopo kata ya Naisinyai Taafa ya Moipo
wilayani humo na kudai kuwa watu wengi wamejikomboa kupitia mikopo wanayopata
kwenye vikundi vya wajasiriamali.
Alisema wajasiriamali wanaweza
kufanikiwa kimaisha kwa kupitia kwenye vikundi kuliko kuwa mtu mmoja mmoja na
aliwatakiwa wasiogope kuchukua mikopo kwenye taasisi za fedha ili waweze
kujiinua kiuchumi na kujikomboa.
“Nawaeleza ukweli tunaposema
maisha bora kwa kila mtanzania inakubidi ujishughulishe kwani maisha bora au
Tanzania yenye neema haitapatikana kwa mtu asipojishughulisha na kujiangaisha
kwa kutoka jasho,” alisema Mandia
Naye,mlezi wa kikundi
hicho,Kilempu Ole Kinoka alisema kikundi cha Jitegemee kilianzishwa Octoba 4 mwaka
2011 kikiwa na wanachama 25 wa jinsia ya kiume na kike huku asilimia kubwa ya
wana kikundi wakiwa jamii ya wafugaji.
Ole Kinoka ambaye pia ni Diwani
wa kata ya Naisinyai alisema lengo la kikundi hicho ni kuondoa umaskini,kuhamasisha
na kutunza mazingira na hadi hivi sasa wamefanikiwa kufungua akaunti yao kwenye
benki ya makabwela ya NMB.
Alisema kikundi hicho
kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na elimu ya
ujasiriamali,ukosefu wa mikopo na wanachama kutokuwa na mitaji ya kuendesha
miradi itakayowasaidia kulea familia zao.
Wajumbe wa kikundi hicho pia
walimpa Mandia,zawadi ya mavazi ya jadi kama kumbukumbu yao kwao,ambapo mkuu
huyo wa wilaya aliwashukuru na kuwaeleza kuwa wanazidi kumuonyesha upendo wao
na atazidi kuwakumbuka.