WACHIMBAJI watatu wakazi wa King’ori
wilayani Arumeru mkoani Arusha,wamefariki dunia kwa kukosa hewa mgodini baada
ya kuingia kwa lengo la kuiba madini kwenye mgodi unaomilikiwa na kampuni ya
TanzaniteOne ya mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Akizungumza
na waandishi wa habari
ofisini kwake jana,Kamanda wa polisi mkoani Manyara,Liberatus Sabas
alisema tukio hilo lilitokea Desemba 28 mwaka huu na aliwataja
marehemu hao ni Afrael Amos (22) Baraka Soine (19) na Simon Laban (32)
wote
wakazi wa King’ori.
Kamanda Sabas alisema walipata
taarifa ya kupotea watu sita walihisiwa waliingia kwa wizi kwenye mgodi huo wa
TanzaniteOne kwa lengo la kuiba madini ya Tanzanite lakini baada ya kuwafukua
imebainika walikuwa watatu.
Alisema baada ya kufukua mgodi huo wa
JW ambao haufanyiwi kazi unaomilikiwa na kampuni ya TanzaniteOne uliopo kitalu
C,walikuta miili hiyo mitatu ikiwa imeharibika sana kutokana na kukaa muda
mrefu mgodini hapo.
Alisema miili ya marehemu hao
imeshachukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya shughuli za mazishi baada ya
uchunguzi wa daktari kufanyika mgodini hapo kwani miili hiyo ilikuwa
imeharibika sana.
Kamanda Sabas alitoa wito kwa
wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite kuchukua tahadhari wanapokuwa
wanachimba madini kwani kazi hiyo ni ya hatari hivyo hawatakiwi kuingia kwenye
migodi isiyotumika.
“Kazi ya kuingia kwa wizi kwenye
mgodi ambao siyo wako siyo nzuri kwani unahatarisha maisha yako kwa kufanya
kazi sehemu isiyo salama kama hao walivyoingia kwenye mgodi usio wao na
usiotumika,” alisema Kamanda Sabas.