IMEELEZWA kwamba Serikali iliyopo madarakani
haipo tayari kuwafukuza wawekezaji wakiwemo wachimbaji wakubwa wa madini ya
Tanzanite hivyo wachimbaji wadogo wanatakiwa kushirikiana nao.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa mkoa wa
Manyara,Elaston Mbwilo wakati akizungumza jana mji mdogo wa Mirerani wilayani
Simanjiro na wadau na wachimbaji wa madini ya Tanzanite.
Mbwilo aliyasema hayo akiwa na Kamati
ya ulinzi na usalama ya mkoa huo na Kamati ya ulinzi na usalama ya Taifa iliyoongozwa
mjumbe wa kamati hiyo Peter Bachubira na lengo lake likiwa kuona hali ya
maendeleo ya wachimbaji mazingira ya uchimbaji,changamoto na mahusiano ya
wachimbaji hao.
Mbwilo amewataka wachimbaji wadogo wa
madini ya Tanzanite kushikiriana na wachimbaji wakubwa wa madini hayo kwani
Serikali inayoongozwa na CCM inawakubali wawekezaji na haitawafukuza.
Alisema Sera ya Serikali ya chama
kilichopo madarakani kinawakubali wawekezaji hao hivyo kama wanataka wawekezaji
hao waondoke wasubiri hadi chama kingine kiingie madarakani.
“Ilani ya Serikali ya CCM inakuwakubali
wawekezaji na siyo kuwafukuza,ombeni mpatiwe vifaa vya uchimbaji na siyo
kumfukuza mwekezaji,lakini kama mnadai Rais aliwaahidi atawapa eneo la
wawekezaji nitamkumbusha,” alisema Mbwilo.
Aliyasema hayo baada ya wachimbaji
wadogo wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama cha wachimba madini wadogo mkoani
Manyara (MAREMA) kudai Rais Jakaya Kikwete aliahidi kuwapa eneo la kitalu C
baada ya leseni yao kumalizika.
Mwenyekiti huyo,Zephania Mungaya
alisema wachimbaji wadogo wanatakiwa kupatiwa eneo hilo kwani hivi sasa
wanachimba kitaalamu na pia sheria ya madini hairuhusu madini ya vito kuchimbwa
na wageni.
Mughaya alisema hivi sasa wanachimba
kitaalamu kwani zaidi ya migodi 40 imefungwa vifaa vya kisasa na ajali za
migodini zimepungua kutoka vifo vya watu 20 kwa mwaka hadi watu sita,wawili au
hakuna kabisa kwa mwaka.
Kwa upande wake Jafari Bakary alisema
usalama wa Taifa watakuja kuulizwa walikuwa wapi wakati mali za Taifa
zikichukuliwa kwani wasimamizi wa Serikali wamechangia Mirerani kuzidi kuwa
nyuma kwa maendeleo.
Bakary alisema wasimamizi wa Serikali
wamechangia mji huo kutopata maendeleo kwani una watu zaidi ya 50,000 lakini
kuna kata mbili pekee hivyo kuzidi kudidimiza maendeleo kwa kutopatiwa mahitaji
ipasavyo.
Naye,Kaanael Minja alisema japokuwa
madini ya Tanzanite yanachimbwa eneo la Mirerani peke yake hapa duniani lakini
maendeleo yaliyopo hayafanani na hazina inayopatikana kwenye eneo hilo.
Minja alisema kwenye machimbo hayo zimefika
tume nyingi za madini lakini hazijawapatia wananchi majibu mazuri lakini wajumbe
hao wanauwezo wa kufikisha ujumbe kwa Rais Jakaya Kikwete kwani ni mtu msikivu
na anayeelewa.