WANAO PELEKA MIFUKO KWENYE MASHAMBA YA WAKULIMA WAKAMATWE

MKUU wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara,Khalid Mandia ameiagiza Serikali ya kijiji cha Ngage,kuwachukulia hatua kali za kisheria wafugaji wa kijiji hicho watakaoingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.

Mandia alitoa agizo hilo juzi,wakati akizungumza na wakulima na wafugaji wa vitongoji vya Ndepes na Olbil,kijiji cha Ngage,Kata ya Loiborsoit,alipofanya ziara yake ya siku moja kijijini hapo kwa lengo la kuhimiza shughuli za maendeleo.

Alisema kijiji hicho kimepimwa na kupangiwa maeneo ya makazi,huduma za jamii,malisho na mashamba,hivyo kila mfugaji anatakiwa kutii sheria kwa kutoruhusu mifugo yake kula mazao ya wakulima yaliyopo mashambani.

“Mmejiwekea sheria ndogo wenyewe,mnapaswa kuzitii na kuzifanyia kazi na kila mifugo inayokutwa kwenye mashamba ikiharibu mazao inatakiwa ikamatwe,itozwe faini na mtu atakayekaidi apelekwe polisi,” alisema Mandia.

Alisema Serikali imetoa fedha nyingi kiasi cha sh492 milioni kwa ajili ya kujengwa mfereji wa kilimo cha umwagiliaji kwa wakazi wa eneo hilo hivyo hatakubali wafugaji waharibu miundombinu hiyo au mazao mashambani.

“Serikali imeacha kupeleka fedha zake kununua dawa na vitabu shuleni ikatenga ruzuku kwa wakulima,ninyi wafugaji mnachungia mifugo mashambani sitakubali na sina utani na mtu nitawaweka ndani, ” alisema Mandia.

Naye,Ofisa Mtendaji wa Kata ya Loiborsoit,Laurent Munga alisema mtu mmoja aliandika barua kwenye gazetini moja na kudai ni wakulima walioandika,wakati kijijini hapo wafugaji huwa wanapigwa faini mifugo yao ikiharibu mazao ya wakulima mashambani.

Munga ambaye pia ni Kaimu Ofisa Tarafa ya Ruvu Remit aliwataja baadhi ya wakulima waliolipwa na wafugaji ni Anna Mariyatabu sh300,000 Esta Mshau sh1 milioni,kikundi cha vicoba sh300,000 na Kiondo alilipwa sh700,00.

“Huyo ni mchochezi mmoja ameamua kutupaka matope kwanza anayefanya kazi ya kuhakiki na kutathmini mazao yaliyoharibika shambani ni Ofisa kilimo siyo watendaji tufanyeni kazi tuache majungu jamani,” alisema Munga.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post