BREAKING NEWS

Wednesday, April 25, 2012

MAJANGILI WATANO WAKAMATWA

WATUMISHI wa Idara ya Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro
Mkoani Manyara wamewakamata majangili watano wakiwa na nyama ya
twiga,meno ya tembo na bunduki zinazotumika kuwindia wanyama pori.

Pia watumishi hao wa idara ya maliasili wamefanikiwa kukamata magari
mawili na pikipiki moja ambayo yametumika kuwindia wanyama pori
wilayani humo pamoja na majangili wengine wadogo wadogo wanaotumia
baiskeli.

Juhudi hizo za watumishi hao wa idara hiyo kukamata majangili hao
inatokana na malalamiko ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo
waliokutana mwaka jana na kuipa idara hiyo muda wa kujirekebisha kwa
kulinda rasilimali hizo.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo walitoa muda wa miezi
miwili kwa watumishi wa idara hiyo kupambana na majangili
wanaojihusisha na uwindaji haramu la sivyo wangewachukulia hatua kali
watumishi hao.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani mwishoni mwa wiki
iliyopita,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo,Patrick Saduka
alisema watuhumiwa hao wa ujangili wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Saduka alisema watumishi hao wa maliasili waliwakamata majangili
watano wakiwa na bunduki mbili za kuwindia tembo (Cork Hand) na meno
mawili ya tembo eneo la Orkugit,pikipiki moja na nyama ya twiga eneo
la Kitwai.

“Pia watumishi hao wa idara ya maliasili walifanikiwa kukamata gari
moja aina ya Land Cruser ZX ikiwa na meno mawili ya tembo na gari moja
aina ya Toyota Hilux likiwa limesheheni nyama ya pori,” alisema
Saduka.

Alisema kwenye eneo la kijiji cha Namalulu walifanikiwa kukamata meno
manne ya tembo na kwenye eneo la Kabojo kata ya Rvu Remit waliyakamata
magari mawili yakiwa na nyama ya pori pamoja na bunduki tatu za
kuwindia.

Alisema pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa
idara hiyo ya maliasili ikiwemo upungufu mkubwa wa vifaa na jiografia
ya ukubwa wa wilaya hiyo bado wanaendelea na mapambano dhidi ya
uwindaji haramu.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates