MSIMAMIZI wa tume ya uchaguzi katika jimbo
la Arumeru mashariki,Trasias Kagenzi amemtangaza ,Joshua Nasari
(26)wa CHADEMA,kuwa mbunge mteule katika jimbo hilo baada ya kuibuka kidedea na
kuwabwaga wenzake saba kutoka vyama mbalimbali vilivyoshiriki uchaguzi
huo.
Akitangaza matokeo hayo le
alfajiri ,Kagenzi alisema kuwa Nasari aliibuka mshindi kwa kupata kura 32,972
sawa na asilimia 54,na kufuatiwa na mgombea wa chama cha mapinduzi ,Sioi Sumari
aliyeambulia kura 26,757 sawa na asilimia 42.
Aidha aliongeza kuwa jumla ya
wapiga kura waliojiandikisha katika jimbo la uchaguzi la Arumeru
mashariki walikuwa ni 127,453,waliopiga kura ni 60,696 ,kura halali zilikuwa
60,036 ,zilizoharibika ni 661.
Kagenzi alisema kuwa vyama vingine
vilivyoshiriki ni AFP ambapo mgombea wake alipata kura 139,UPDP kura 18,TLP kura
18,SAU 22,NRA 35 na DP kura 77,hata hivyo alifafanua kuwa hali ya
uchaguzi ilienda vizuri kwani hakukuwapo na malalamiko mengi katika kipindi cha
kampeni hadi kupiga kura ,ambapo wakazi mbalimbali walijitokeza na kushiriki
kikamilifu katika zoezi hilo.
Msimamizi huyo mara baada ya
kutangaza matokeo hayo alivishukuru vyama vya siasa vilivyoshiriki
kinyang’anyiri hicho cha uchaguzi, akidai vimeonyesha ukomavu wa hali ya juu
licha ya ya kasoro na dosari ndogo ndogo zilizojitokeza na kutoa wito kwa vya
vya siasa kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la upigaji kura ili kuondoa
malalamiko pindi mshindi anapotangazwa kwa madai kuwa matokeo
yamechakachuliwa.
Alivitaka vyama vya siasa kuiamini
tume ya uchaguzi kwani hatua ya kuchelewesha matokeo hatokei maksudi kwa lengo
la kutoa ushindi wa mezani kwa vyama vingine ila kinachofanyika ni taratibu za
kuhakiki masanduku ya kura pamoja na fomu za mawakala,hiyo
aliwasihi wafuasi wa vyama vya siasa kuacha kuitumia lawama ofisi ya msimamizi
wa uchaguzi na kutishia kumvamia kwa lengo la kushinikiza matokeo yatangazwe
haraka.
‘’wafuasi wa vyama ni vema wawe
wavumilivu kwani hatua ya kupiga kelele na kutaka wapatiwe matokeo haraka
,yanakuwa hayana maana kwani utaratibu wa sasa tunatumia vyombo vya kisasa
katika kuhakiki matokeo kwa kutumia kompyuta ‘projector’alisema
Kagenzi
Akizungumza muda mfupi baada ya
kutangazwa matokeo hayo,Nasari pamoja na kuwashukuru wapiga kura wake kwa
kumchagua ,aliipongeza tume ya uchaguzi kwa kusimamia vema uchaguzi huo kwani
hali hiyo imeondoa malalamiko mengi na pengine yangewea kuibua
machafuko na uvunjivu wa amani.
Nasari alisema kuwa kazi iliyombele
yake ni kuhakikisha anarudisha fadhila kwa wapiga kuwa wake ambao wamemwamini na
kuamua kumchagua kwa kuwatumikia ,ambapo alitangaza kuanza kazi mara moja ya
kuchimba visima viwili katika kata Maroroni ambako kuna shida kubwa ya uhaba wa
maji.
Katika hatua nyingine Nasari
alitaka jeshi la polisi kuwaachia huru wafuasi wa chadema zaidi ya 70
anaoamini ni wapiga kura wake, wanaoshikiliwa katika kituo kikuu
cha Arusha kutokana na vurugu zilizozuka eneo la mji mdogo wa Usa River baada ya
wafuasi wa chadema kuzingira barabara na kuzuia magari kuingia eneo la kuhesabia
kuwa na kusababisha kupigwa mawe na kuvunjwa vioo kwa gari la
kifahari la naibu kamishina wa jeshi la polisi nchini ,Isaya
Mgulu,lenye namba za usajiri T 859 BWB.
Katika vurugu hizo jeshi la polisi
lililazimika kuwatawanya wafuasi hao kwa kuwafyatulia mabomu ya machozi majira
saa 3 usiku hadi saa 5 ,ambapo polisi iliamua kutumia sialaha za moto na mabomu
kuwatawanya wafuasi hao waliokuwa na jazba wakizuia gari la aina yoyote kupita
na kwenye eneo la chumba cha majumuisho wakidai yanapitisha kura chafu kwa lengo
la kuchakachua matokeo.
Polisi ilifanikiwa kuwatia mbaroni
wafuasi zaidi 70 wa chadema na wanashililia katika kituo cha
polisi mjini Arusha ,hadi asubuhi walikuwa bado
wakiendelea kutoa maelezo kituoni hapo.
|