BARAZA LA MADIWANI SIMANJIRO LAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 13

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani
Manyara limepitisha bajeti yake ya sh13.5 bilioni ikiwa ni mapato kwa
mwaka wa fedha wa 2012/2013.

Akisoma bajeti hiyo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani,Mtunza
Hazina wa halmashauri hiyo,Peter Mollel alisema fedha hizo ni kwa
ajili ya miradi ya maendeleo,ruzuku ya mishahara na matumizi ya
kwaida.

Mollel alisema bajeti hiyo imelenga kufanikisha vipaumbele mbalimbali
vya elimu,afya,maji,miundombinu ya barabara na ujenzi wa nyumba za
walimu na madarasa katika kata 18 za halmashauri ya wilaya hiyo.

Alisema kuwa katika fedha hizo sh1.3 bilioni na sh2.8 bilioni ni fedha za
maendeleo sh1.8 bilioni na sh7 bilioni ni ruzuku ya mishahara na
matumizi ya kawaida na sh1. bilioni ni mapato ya ndani.

Alisema bajeti ya kipindi hiki imeongezeka kutoka sh 9 bilioni kwa
mwaka wa fedha wa 2011/2012 kuwa sh13.5bilioni,hivyo kutakuwa na
maendeleo makubwa yatakayotekelezwa kwa kushirikiana na nguvu za
wananchi.

Akizungumza kwenye Baraza hilo,Diwani wa kata ya Mirerani Justin Nyari
aliitaka idara ya uchumi na mipango ya halmashauri hiyo kutoidhinisha
miradi mipya wakati ambapo miradi iliyoibuliwa awali ikiwa bado
haijakamilika.

“Hili ni tatizo la kata nyingi ambapo miradi ambayo haijakamilika
inaibuliwa miradi mingine hivyo mipango wanapaswa kuipa kipaumbele
miradi hiyo kuliko kuibua mipya kabla ya kumalizika kwa miradi ya
viporo,” alisema Nyari.

Alisema baadhi ya miradi ya madarasa ya shule za msingi na
sekondari,nyumba za walimu,zahanati na barabara imekuwa ikiachwa
viporo kabla ya kumaliziwa na kuibua miradi mipya hivyo kufifisha
maendeleo ya sehemu husika.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post