JESHI la Polisi Mkoani Manyara
linamshikilia mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite,Elitabu Mkenga (39)
kwa kudaiwa kuwatishia na bastola polisi wa Mirerani walioingia kukagua mgodi
wao unaodaiwa kuua mchimbaji wa mgodi mwingine kwa baruti na kujeruhi
wachimbaji wawili.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa polisi
mkoani Manyara,Eurelia Msindai tukio hilo lilitokea kwenye eneo la machimbo ya Tanzanite kitalu “B” (Opec) mji mdogo wa
Mirerani wilayani Simanjiro.
Kaimu Kamanda Msindai alisema
mchimbaji aliyekufa na waliojeruhiwa ni wafanyakazi wa mgodi wenye PML namba
0001393/96 wa kampuni ya Building Utilties unaomilikiwa na Simon Meshak mkazi
wa mkoani Arusha.
Alimtaja mchimbaji huyo aliyefariki
ni John Alex (36) mkazi wa Sanawari mkoani Arusha ambaye baruti hiyo ilimkata
mkono wa kuume,utumbo ulitoka nje na mguu wa kuume ulikatika kwenye ajali hiyo.
Aliwataja majeruhi hao ni Jeremia
Ramadhan (34) mkazi wa Mirerani aliyejeruhiwa bega la kuume,kifua na John
Daimon (25) mkazi wa Kazamoyo Mirerani
aliyejeruhiwa goti la kushoto.
“Baada ya wachimbaji hao kulipuliwa
na baruti viongozi wa mgodi walitoa taarifa kituo cha polisi Mirerani kuwa
mgodi unaomilikiwa na John Mkenga wenye PML 00000021 ndiyo ulisababisha ajali
hiyo,” alisema Msindai.
Alisema polisi walipofika mgodini
hapo waliokuwa kwenye mgodi wa Mkenga waligoma kufungua geti wakidai kuwa ndugu
wa mmiliki,Elitabu Mkenga ana ufunguo,ndipo polisi wakatumia nguvu na kuingia
ndani ya mgodi huo.
Alisema polisi walipoingia Elitabu
Mkenga (39) ambaye ni mdogo wa mmiliki wa mgodi huo na mfanyabiashara maarufu
wa madini ya Tanzanite wa mjini Arusha aliwatishia askari hao kwa kupiga risasi
hewani kwa kutumia bastola yake.
Kaimu Kamanda Msindai alisema polisi
hao wakiongozwa na msaidizi wa Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani Mkaguzi wa
polisi Wenceslaus Gumha na askari wapelelezi Isack na Allen walitishiwa na Elitabu
Mkenga na bastola aina ya brown.
“Hata hivyo polisi walifanikiwa
kumtia mbaroni na hadi hivi sasa yupo mahabusu kituo cha polisi Mirerani na
anatarajia kufikishwa Mahakamani baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika,”
alisema Msindai.
Kaimu Kamanda Msindai alisema mwili
wa marehemu huyo umehifadhiwa kwenye hospitali ya mkoa wa Arusha Mount Meru na
majeruhi hao nao wamelazwa kwenye hospitali hiyo ya Mount Meru.