JUMLA ya kiasi cha $
80,000 zikiwemo ahadi ambazo ni kiasi cha sh,10.5 milioni zimepatikana
katika harambee ya kuchangia mfuko wa kuwawezesha wanawake ambao
ni wachimbaji madini mkoani hapa huku kampuni kubwa ya uwekezaji ya madini ya
Tanzanite One ikichangia jumla ya $ 20,000.
Fedha hizo zilichangwa mwishoni mwa
wiki iliyopita kwa lengo la kuwawezesha wanawake ambao ni wachimbaji madini
mkoani ili waweze kupatiwa elimu ya uchimbaji madini sanjari na mbinu za ukataji
wa madini,vito na upambaji kwa ujumla.
Akizungumza kabla ya kuzindua zoezi
la uchangishaji wa fedha hizo mgeni rasmi ambaye ni waziri wa nchi ofisi ya
waziri mkuu uwekezaji na uwezeshaji ,Dk Mary Nagu alisema kwamba pamoja na
kwamba asilimia kubwa ya wanawake nchini kuwa ni watuamiaji wa
vito na madini mbalimbali lakini wengi wao hawanufaiki kupitia sekta
hiyo.
Alisema kwamba asilimia kubwa ya
wanawake wengi nchini wanaojishughulisha na biashara ya madini mbalimbali hawana
elimu ya kutosha kuhusiana na uchimbaji wa madini hivyo fedha hizo zitasaidia
katika kuwawezesha kupatiwa elimu ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi
mkubwa.
“Hakuna kitu kitakachowakwamua
wanawake nchini zaidi ya elimu,kama tukiwakwamua wanawake basi tujue tumeikwamua
jamii kwa ujumla na watafanya vizuri zaidi”alisema Nagu
Naye,mwenyekiti wa bodi ya kampuni
uchimbaji madini ya Tanzanite One iliyopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara,Ami
Mpungwe alisema kwamba wao kama wadau wakubwa wa sekta ya madini nchini wameamua
kuwakwamua wanawake waliopo ndani ya sekta hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo
nchini.
Alisema kwamba ni wajibu wa kila mdau
aliye ndani ya sekta hiyo kuwakwamua wanawake mbalimbali wanaojishughulisha na
biashara hiyo ya madini kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi na kupunguza umaskini
uliokithiri ndani ya jamii mbalimbali za kitanzania.
“Sisi kama Tanzanite One ni wajibu
wetu kuwasaidia wanawake wote walioko ndani ya jamii hususani wachimbaji wa
madini,tuko kwa ajili ya kusaidia kuinua uchumi wa nchi kuleta maendeleo
”alisema Mpungwe ambaye aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Afrika
kusini
Awali katibu mkuu wa wizara ya
nishati na madini nchini,Eliakim Maswi alisema kwamba wizara yao itashirikiana
bega kwa bega kuhakikisha inasaidia kuandaa na kuboresha
maonyesho makubwa ya madini na vito kila mwaka.
|