WANANCHI wa kijiji cha
Olgilai kata ya Oltoroto wilayani Arumeru mkoani Arusha wameiunga serikali mkono
katika swala la upanuzi wa barabara ambao ulikuwa ukisua kwa muda
mrefu kutokana na baadhi ya wananchi kutoafiki swala hilo na hivyo kupelekea
zoezi hilo kusitishwa .
Hata hivyo uamuzi huo umekuja baada
ya wananchi hao pamoja na viongozi ngazi ya kijiji, kuafikiana kwa
pamoja na kukubali kupisha upanuzi wa barabara katika kijiji hicho
unaofanywa na halmashauri ya Arusha vijijini.
Aidha wananchi hao wamekubaliana
katika mkutano mkuu wa kijiji cha Olgilai uliowashirikisha wananchi mbalimbali
kutoka kijiji hicho uliolenga kujadili agenda mbalimbali kubwa zaidi ikiwa ni ya
upanuzi wa barabara kutoka Sekei hadi Olgilai.
Hata hivyo wananchi hao kwa pamoja
na viongozi mbalimbali wa kijiji walikubaliana kupeana muda wa wiki moja
kuhakikisha kuwa kila mwananchi awe ametoa fensi katika eneo hilo,
geti, na mazao mbalimbali yaliyoko ili kupisha upanuzi wa barabara ambao utaanza
mapema tu watakapomaliza zoezi hilo.
Aidha kikao hicho ambacho
kiliendeshwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho,Jackson Boaz kwa
kushirikiana na Mtendaji wa kijiji hicho , Mathias Mollel ambapo wananchi
mbalimbali walieleza maoni yao kuhusiana na upanuzi huo wa barabara ikiwemo la
kuomba kulipwa fidia kwa wananchi watakaovunjiwa nyumba zao kupisha upanuzi
huo.
Ambapo wananchi hao kwa nyakati
tofauti wkichangia mada hiyo walisema kuwa, wao kwa ujumla wanapenda maendeleo
sana katika kijiji chao ila wangeomba serikali iweze kuwafidia
wale ambao watabomolewa nyumba zao huku ikilinganishwa kuwa sio nyumba nyingi
zitakazopitiwa katika upanuzi huo wa barabara.
Wakichangia kwa nyakati tofauti mada
hiyo, wananchi hao ambao ni Godwin Masangwa na Gadiel Losoroye
walisema kuwa, swala zima la upanuzi wa barabara limekuwa likileta
maswali sana kwa wananchi walio wengi katika kijiji hicho ambapo
wengi wao wamekuwa wakitaka kujua hatma ya nyumba zao zitakazobolewa kupisha
upanuzi huo wa barabara.
Ambapo walisema kuwa
,walishawahi kuandika barua kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo wakiomba
kufikiriwa wananchi ambao nyumba zao zitabomolewa
angalau walipwe fidia kutokana na kuwa walijenga nyumba hizo kipindi ambacho
sheria hiyo ya upanuzi wa barabara ilikuwa haipo na hawakujua kuwa hilo ni eneo
la barabara.
Wakisomewa barua iliyojibiwa na
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Halifa Ida ambayo inasema kuwa, wao kama
halmashauri hawana fedha zozote za kuwalipa fidia wananchi watakaobolewa nyumba
zao , kwani hadi sasa hivi wamekwisha pokea kiasi cha shs 100 milioni kutoka
mfuko wa barabara kwa ajili ya upanuzi wa barabara hiyo ya kutoka
Sekei hadi Olgilai kwa kiwango cha changarawe.
Naye Mwakilishi wa mhandisi kutoka
halmashauri ya Arusha vijijini, Frank Mwanga alisema kuwa, wanachopaswa kujua
wananchi ni kuwa kwa sasa hivi upanuzi wa barabara utafanyika
katika mita 7.5 kwa 7.5 kutoka upana wa barabara .
Alisema kuwa , wananchi wanapaswa
kujua kuwa , hifadhi ya barabara ni mita 20.5 kutoka upana wa
barabara ambapo kwa sasa hivi wanapanua barabara ili kuwezesha magari mawili
kupishana ambapo wataanza na mita 7.5 tu, hivyo
wananchi wanachopaswa kujua ni kuhakikisha kuwa wanakuwa makini
wanapotumia mita hizo huku wakijua kuwa ni hifadhi ya barabara na
itatumika wakati wowote.
Aidha barabara itakayopanuliwa ni
kilometa 5.3 kutoka sekei kata ya Sokon 1 hadi kijiji cha Olgilai kilichopo kata
ya Oltoroto .
Diwani wa kata ya Oltoroto ,Gibson
Meseiyeki alipongeza uamuzi wa wananchi wake kufikia hatua ya kuunga mkono swala
hilo la maendeleo kwani inaonyesha wazi ni jinsi gani wanawaunga mkono viongozi
wao na ni mfano wa kuigwa kwa wananchi wengine.
Alisema kuwa, wananchi wengi
wamekuwa ndio kikwazo kikubwa cha kuwakatisha tamaa viongozi
mbalimbali wanapobuni miradi , kutokana na kutounga mkono miradi
hiyo, hivyo aliwataka wananchi hao ambao wapo kwenye hifadhi ya barabara
kutoendeleza shughuli zozote ili kupisha upanuzi huo wa barabara na kuondokana
na usumbufu mbalimbali.