IKULU YAKANUSHA MATAMSHI YA GODBLESS LEMA KUHUSIANA NA KUENGULIWA KWAKE.
Katika mahojiano yake leo, Alhamisi, Aprili 5, 2012, na Redio One, ikiwa ni kauli yake ya kwanza baada ya Mahakama Kuu ya Arusha kutangaza kumvua ubunge, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Bwana Godbless Lema, amedai kwa jazba sana kuwa hukumu ya Mheshimiwa Jaji Gabriel Rwakibalira imetokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Ikulu.
Kauli hii ya Bwana Lema ni upuuzi. Siyo Mheshimiwa Rais Kikwete wala Ikulu imeingilia kati kesi yake kwa namna yoyote ile, iwe ni kwa kupiga simu ama kuzungumza na Mheshimiwa Jaji Rwakibalira.
Kwa hakika, haijapata kutokea Mheshimiwa Kikwete, tokea alipoingia madarakani, Desemba 21, 2005, akaingilia, kwa namna yoyote ile, mwenendo wa kesi yoyote ile katika Mahakama yoyote na ya ngazi yoyote katika Tanzania. Na wala hakusudii kufanya hivyo wakati wote wa muda wake uliobakia wa uongozi. Siyo kazi ya Rais kutoa hukumu ama kuelekeza namna ya kutoa hukumu katika kesi zilizoko Mahakamani. Rais hana madaraka wala mamlaka hayo.
Aidha, kauli ya Bwana Lema ni ukosefu mkubwa wa adabu na heshima kwa Mahakama ambao ni Muhimili Huru usioingiliwa na Serikali ama na Muhimili mwingine katika maamuzi yake. Bwana Lema amekuwa kiongozi kwa muda sasa, hivyo ni lazima atambue jambo hili kubwa na muhimu katika mfumo mzima wa utawala wa nchi yetu.
Ni jambo lisilokuwa na mshiko wala tija, na kwa kweli ni bahati mbaya, kwamba Bwana Lema anajaribu kuingiza mambo yasiyohusika katika jambo la dhahiri kabisa kuwa ni la kisheria ambalo msingi ni hoja na maelezo mahakamani.
Bwana Lema asitafute visingizio kwa yaliyomfika kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kumbebea msalaba huu. Badala ya kutafuta mchawi asiyekuwepo, ni vyema Bwana Lema angekaa chini na kuangalia ni sababu zipi za kisheria zilizomfanya ashindwe na kama ameridhika kuwa hakutendewa haki akate rufani kwa mujibu wa sheria na taratibu. Tunaomba wananchi wampuuze. Ameshindwa kesi kwa makosa yake aliyofanya hana mtu wa kumlaumu bali ajilaumu mwenyewe
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia