HALMASHAURI za Wilaya za Mikoa ya Manyara na
Kilimanjaro zenye mabwawa na maziwa zimetakiwa kutunga sheria ndogo za kudhibiti
uvuvi haramu kwa lengo la kustawisha uvuvi endelevu na wenye
tija.
Azimio hilo limetolewa na kamati ya
Ulinzi na Usalama ya mikoa ya Manyara na Kilimanjaro walipokutana mji mdogo
wa Mirerani wilayani Simanjiro kwenye kikao cha ujirani mwema cha kujadili Bwawa
la Nyumba ya Mungu.
Bwawa hilo la Nyumba ya Mungu
linalopatikana kwenye wilaya za Simanjiro Mkoani Manyara na Mwanga na Moshi
mkoani Kilimanjaro,kutokana na kukithiri uvuvi haramu hivi sasa limefungwa hivyo
kusitisha shughuli za uvuvi.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas
Gama alisema halmashauri zinatakiwa zisimamie vijiji vyenye ziwa au bwawa ili
vitunge sheria ndogo za kusimamia rasilimali hizo ili kwenda sambamba wakati wa
usitishaji wa uvuvi.
Gama ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa
kamati hiyo alisema vijiji vinaweza kutunga sheria hizo ndogo kwa haraka na
kisha zikaidhinishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya tofauti na sheria za
halmashauri zinazochukua muda.
Mwenyekiti wa kikao hicho,Mkuu wa
mkoa wa Manyara Elaston mbwilo alisema kuna haja ya kuungana na mkoa wa Arusha
katika kudhibiti uvuvi haramu kwani kuna baadhi ya watu wanadai wanatoa samaki
ziwa Eyasi.
“Lile ziwa tunatambua kuwa ni lina
chumvi sasa wafanyabiashara wa samaki wanatumia fursa ya kupata samaki kwenye
maeneo mengine wanasingizia wamevua kwenye ziwa hilo ambalo halijafungwa kwa
uvuvi,” alisema Mbwilo.
Naye,Mkuu wa wilaya ya
Simanjiro,Khalid Mandia aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa baadhi ya wavuvi
haramu wanatangaza kuwa japo amelifunga Bwawa la Nyumba ya Mungu lakini funguo
ameziangusha na wao wameziokota.
“Wanadai kuwa kutokana na hali hiyo wao
wanaendelea kuvua samaki nyakati za usiku wa manane,hivyo tujitahidi kuweka
fungu lakutosha kwa ajili ya askari wa doria watakaolinda bwawa hilo nyakati za
usiku,” alisema Mandia.
Alisema bila kufanya hivyo zoezi la
kufunga bwawa hilo na kusitisha uvuvi halitaweza kuwa na tija kwani wavuvi
haramu wataendelea kuvua samaki wadogo na kuzorotesha ustawi wa samaki wa bwawa
hilo