Gari ya mahabusu
WAKILI maarufu nchini, Median Mwalle amewasihi mawakili
wa serikali kuhakikisha wanasoma sheria na kuzielewa pamoja na kujipanga kujibu
hoja ili kuondoa malalamiko ya ucheleweshwaji wa kesi mbalimbali mahakamani.
Mwale aliyesema hayo mbele ya
Jaji, Kakusulo Sambo wa mahakama kuu kanda ya Arusha,wakati
alipokuwa akitetea hoja za mapingamizi yake matano aliyoyawasilisha
mahakamani hapo dhidi ya kupinga hatua ya mawakili wa serikali kupeleka
shauri Mahakama Kuu ili lipitiwe upya kwa madai ya kutoridhishwa na
uamuzi uliotolewa na Hakimu Charles Magesa juu ya kurudishiwa magari yake ya
kifahari yanayoshikiliwa na serikali.
Mwale alisema pingamizi alizoziwasilisha
awali mahakamani hapo juu ya kupinga maamuzi ya kutorudishiwa magari yake ya
thamani hayakuwa sahihi kwa serikali na hayana mashiko hivyo aliiomba mahakama
hiyo ione kuwa maombi yake ni ya msingi na anastahili kukabidhiwa magari
yake.
Alisema hoja walizozitoa mawakili wa serikali hazina msingi pia hazina baadhi ya viambatanisho vinavyoweza kuishawishi mahakama hiyo kutomrudishia magari yake yanayoshikiliwa katika ofisi za TRA jijini Arusha.
Wakili Mwalle alidai kuwa upande wa serikali hawakupaswa kuchukua hatua hiyo kwani uamuzi uliofanyika haukuwa wa mwisho wa kumaliza shauri la msingi lililoko mahakamani na kusisitiza kuwa sheria kifungu cha 372 walichotumia kupeleka shauri hilo mahakama kuu kwa ajili ya marejeo hakipo kwenye sheria za hapa nchini wala haijawahi kutungwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Wakili huyo alidai marejeo hayo yanakosa sifa hasa ikizingatiwa kuwa upande wa serikali umeshindwa kuambatanisha maamuzi ambayo wanaona hawakuridhika nayo kwenye huo uamuzi mdogo .
Mwalle , alidai kuwa mkurugenzi wa
mashitaka nchini (DPP) hana mamlaka kisheria ya kuiwakilisha Mamlaka ya Mapato
Nchini (TRA) kwani ni taasisi hiyo ni huru yenye mawakili wake wa kuwatetea
.
Katika pingamizi hilo waliambatanisha barua za
mawasiliano toka ofisi ya Mkurugenzi wa upelelezi na makosa ya jinai nchini
(DCI) iliyosainiwa na kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) , E S A Mmari kwenda
kwa Kamishina Mkuu wa TRA akimuomba ayahifadhi magari ya Mwalle .
Aidha wakili huyo wa Mwalle kwenye pingamizi hilo
aliloliwasilisha mahakamani kwa njia ya maandishi aliambatanisha barua nyingine
iliyoandikwa na mkurugenzi wa mashitaka nchini nchini na kusainiwa na Fredrick
manyanda kwa niaba yake kwenda kwa hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi ,
Charles Magessa aliyekuwa anasikiliza shauri hilo .
Mwalle alikuwa akitoa hoja zake kumshawishi Jaji Sambo
akubali maombi yake hayo na kutupilia mbali maombi ya mawakili wa serikali
kuzuia magari yake kurudishiwa , huku akitoa mifano ya kesi mbalimbali
zinazofanana na kesi hiyo zilizotolewa maamuzi na majaji mbalimbali ndani na nje
ya nchi.
Baada ya Mwale kutoa hoja zake nzito ,wakili wa serikali
, Neema Ringo aliomba mahakama hiyo kuwapa muda hadi Mei 2 mwaka
huu ili waweze kupitia hoja za wakili Mwalle kwani ametumia vifungu vya sheria
vinavyohitaji kuvijibu kwa hoja za kisheria na si kukurupuka kuzijibu.
Awali serikali iliamua kwenda mahakama kuu
kuomba kupitiwa upya uamuzi wa mahakama ya Hakimu Mkazi wa
kumrejeshea mtuhumiwa huyo magari yake saba.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji
Kakusulo Sambo aliamuru upande wa mashtaka kuandaa na kuwasilisha majibu yao Mei
2 mwaka huu , ili shauri hilo lisikilizwe na kuamuliwa na hatimaye
Mwale aweze kuendelea na kesi nyingine inayomkabili .
Mawakili hao wa
serikali walikata rufaa Mahakama Kuu wakitaka ipitie maamuzi yaliyofanywa na
mahakama hiyo yakiwaagiza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DPP), Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha
kuyarudisha magari saba na simu za mkononi kwa wakili huyo anayetuhumiwa
kupatikana na fedha chafu.
Uamuzi huo
ulitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Magesa, ambaye alisema baada ya kupitia
ushahidi wa pande zote, mahakama yake imeridhika kuwa mamlaka hizo zilikamata
magari hayo kinyume cha sheria ya matunda ya uhalifu (Proceeds Crimes Act)
pamoja na vifungu namba 41 na 44 vya sheria ya mwenendo wa kesi za
jinai..
Magari
yaliyoamriwa na mahakama kurejeshwa kwa Mwale ni T 690 BEW aina ya Range Rover,
T 643 BTS Land Rover Discovery, T 907 BTS BMW, T 118 BRS Cadillac Escalade, T
499 APX Land Cruiser, T 520 BBJ BMW, ambayo yalichukuliwa Novemba mosi, pamoja
na gari T 660 BCG Toyota Chaser lililokamatwa Desemba 8, mwaka
jana.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia