BREAKING NEWS

Monday, April 16, 2012

WANAFUNZI WALALAMIKIA UMBALI WA KUFUATA MAJI

WANAFUNZI wa shule ya sekondari Ewong’on iliyopo kijiji cha Kambi ya
Choka Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wamelalamikia kitendo cha
kufuata maji umbali mrefu hadi kusababisha mwanafunzi mmoja kung’atwa
na nyoka.

Wakizungumza na libeneke la kaskazini,wanafunzi hao ambao majina
yao tunayo walidai kuwa japokuwa wazazi wao wamechangi sh5,000 kwa
ajili ya gharama ya maji yanayochotwa na trekta lakini wao ndiyo
wanachota maji hayo.

Walidai kuwa mwishoni mwa mwezi Machi,mwanafunzi wa kidato cha tatu
Raymin Yasini alingatwa na nyoka mguuni baada ya kwenda kuchota maji
yaliyopo umbali wa kilomita mbili kisha akapewa dawa za kienyeji.

“Kuna chemchem iliyopo mto Rundugai huwa tunakwenda kila saa 11
alfajiri kufuata maji na pia tunatumwa porini kuchanja kuni
tusipofanya hivyo tunanyimwa chakula,” alisema mmoja kati ya wanafunzi
hao.

Aidha,mmoja kati ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo Hamis
Kidodoma (56) alidai kuwa hivi karibuni mtoto wake alichomewa nguo na
kiranja na wasimamizi wa shule hiyo bila sababu ya msingi.

“Yaani kwa sababu mtoto wangu hana shuka za kimasai ndiyo achomewe
nguo zake na mimi baada ya kuchunguza nilibaini kuwa zaidi ya
wanafunzi 33 wa shule hiyo walichomewa sare zao,” Kidodoma.

Wanafunzi hao walidai kuwa chanzo cha kuchomwa moto kwa nguo zao ni
kiranja huyo na msimamizi huyo kudai kuwa nguo na viatu vinapaswa
kuwekwa kwenye bati la chuma na siyo pembeni ya vitanda vilivyopo
bwenini.

Wameiomba Serikali kuchukua hatua kwa uongozi wa shule hiyo kwani
vitendo vingi visivyo vya kistaarabu na vya kikatili vinafanyika kwa
wanafunzi hao bila viongozi wa shule hiyo kuchukua hatua thabiti.

Hata hivyo,akizungumza kwa njia ya simu jana,Kaimu Mkuu wa shule hiyo
Daniel Thomas alidai kuwa hakuna mwanafunzi yeyote kwenye shule hiyo
ambaye aligongwa na nyoka wakati akienda kuchota maji.

Alisema baada ya mashine ya kuvuta maji kuharibika waliamua kuwaagiza
wanafunzi wawe wanachota maji umbali wa mita 200 kutoka eneo la shule
na suala la watoto kuchanja kuni alisema halipo

Thomas pia alikanusha vikali vitendo vya wanafunzi kuchomewa nguo zao
na kudai kuwa wanafunzi wanaobainika hawakuvaa sare za shule,nguo hizo
huifadhiwa mahali na siyo kuchomwa moto na kiranja na msimamizi.

“Hilo jambo halipo japo kuna mzazi alileta taarifa ya nguo za mtoto
wake kuchomwa moto na tukamtaka alete majina ya wahusika ili
tuwashughulikie na hadi hivi sasa bado tunamsubiri atuletee majina
hayo,” alisema Thomas.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates