MKUU wa Mkoa wa Manyara,Elaston Mbwilo
amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwenye sensa ya watu na makazi
itakayofanyika Agosti 26 mwaka huu,ikiwa ni baada ya miaka 10 sensa kufanyika
mara ya mwisho mwaka 2002.
Akizungumza na waandishi wa habari
,Mbwilo alisema sensa hiyo inalengo la kukusanya takwimu za
kiuchumi na kijamii,ajira,vizazi na vifo,elimu na hali ya makazi ya watu wote
wanapoishi nchini.
Alisema kuwa takwimu za sensa hiyo
zitasaidia kuimarisha utawala bora na ukuaji demokrasia,kuamua mipaka mipya ya
majimbo ya uchaguzi na mipaka mingine ya kiutawala.
Alisema takwimu na taarifa
zitakazopatikana katika zoezi hilo,zitasaidia kwenye utekelezaji wa dira ya
Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025 na kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa
MKUKUTA.
“Viongozi wa kada mbalimbali
mnatakiwa kutumia mikutano yenu na wananchi kwa kuwaelimisha
umuhimu wa kujitokeza na kutoa ushirikiano kwenye zoezi la sensa ya watu
na makazi mpaka lifanikiwe,” alisema Mbwilo.
Naye,Mratibu wa Sensa ya watu na
makazi wa mkoa huo,Juma Shaban alisema changamoto kubwa inayowakabili kwenye
mpango wa sensa ni namna ya kuishirikisha jamii mapema kutambua umuhimu wa
kuhesabiwa.
Shaban alisema jamii nyingi hasa za
wafugaji wa wilaya za Kiteto na Simanjiro pamoja na jamii ya wahadzabe wa bonde
la Yaeda Chini wilayani Mbulu ni maeneo ya kupatiwa elimu kikamilifu ili
washiriki vema zoezi hilo.
“Hata hivyo mkoa wa wetu wa Manyara
umejipanga kikamilifu kukabiliana na changamoto hiyo ya kuhamasisha jamii hizo
kupitia viongozi wao wa kimila ili waweze kutambua umuhimu wa sensa ya watu na
makazi,” alisema Shaban.