Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye ufunguzi wa mkutano mkubwa wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameitaka jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na majangili wanaomaliza tembo kwa lengo la kupata pembe zao.
Alisema kutokana na biashara nzuri ya pembe hiuzo duniani majangili wamekuwa na soko tayari kiasi cha kuendeleza vitendo vyao.
Alisema mitandao iliyopo inawezesha kuuawa kwa tembo hao na kufikishwa bidhaa za pembe katika soko haramu ambalo lipo duniani na hivyo bila ushirikiano wa kimataifa wanyama hao ambao ni urithi wa dunia watatoweka kabisa katika miaka ijayo.
Amesema takwimu zilizopo sasa nchini za tembo zinatisha.
Alisema mathalani kwa ujangili pekee kwenye mfumo wa ekolojia wa Selou-Mikumi tembo waliobaki ni 13,084 kwa mwaka jana kutoka Tembo 109,419 waliokuwepo mwaka 2006.
Alisema mfumo uliopo wa ujangili na soko la bidhaa hizo unafanya vita inayoendeshwa na Tanzania kuwa ngumu kama haitapata ushirikiano na mataifa mengine.
Alisema kutokana na ukweli huo wanataka mataifa jirani na jumuiya ya kimataifa kuingia katika mapambano ya kudhibiti biashara hiyo na hivyo kuwamaliza majangili na kuendelea kuhifadhi Tembo.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwenye ufunguzi wa mkutano mkubwa wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori, alisema serikali ya Tanzania imeanzisha mchakato wa kulinda wanyama pori.
Baadhi ya wadau kutoka nchi mbalimbali wanaohudhiria mkutano huo akiwemo Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto).
Mchakato huo ni pamoja na kuimarisha doria , kuendesha operesheni za kukabiliana na ujangili.
Alisema pamoja na kuwapo kwa juhudi za makusudi za kukabiliana na ujangili serikali ya Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kifedha na raslimali watu.
Aidha kumekuwepo na ushiriki mdogo kutoka kwa wananchi katika vita dhidi ya ujangili.
Alisema kutokana na haja ya kukabili ujangili na kuwa na hifadhi endelevu, Februari mwaka huu mataifa ya Botswana, Chad, Garbon na Ethiopia yalitiliana saini mkataba wenye lengo la kupunguza mahitaji ya bidhaa za wanyamapori, kuimarisha sheria zilizopo dhidi ya ujangili na pia hifadhi na kusaidia maendeleo ya maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya uwindaji haramu.
Rais Kikwete alisema katika hotuba yake kwamba kuwepo kwa mataifa hayo katika mkutano huo ni kuendeleza makubalino ya kutojishughulisha na biashara za bidhaa za wanyamapori kwa miaka 10 au hadi hapo tembo waliopo bara la Afrika watakapokuwa wameondoka katika hatari ya kuangamizwa katika uso wa dunia na majangili.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, akizungumza kwenye mkutano mkubwa wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori uliofunguliwa rasmi leo jijini Arusha kwenye ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha rais alisema kwamba mkutano huo wa Arusha unatarajiwa kuona namna ya kuendelea utekelezaji wa makubaliano ya London, Uingereza ya hifadhi ya wanyamapori walio katika hatari ya kutoweka akiwemo Tembo.
Alisema kutokana na mfumo wa ikolojia na hifadhi ya wanyama na majirani zake, Tanzania inataka majirani kushiriki katika kulinda na kuhifadhi ikolojia hiyo na wanyama waliopo na sio kuiachia Tanzania pekee.
Tanzania ikiwa na eneo la kilomita za mraba 943,000 asilimia 30 ya eneo lake na 15 imetumika kwa hifadhi ya wanyamapori na misitu.
Amesema eneo hilo hutumiwa zaidi kwa ajili ya utalii wa wanyamapori ambapo asilimia 17 ya pato la taifa linatokana na utalii huo.
Wakati huo huo Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez ,ameipongeza Tanzania kwa kuitisha kikao cha kujadili ujangili na uhifadhi endelevu wa misitu.
Mwenyekiti wa mkutano mkubwa wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori ambaye pia ni Makamu mwenyekiti wa ICCF Group, Dr. Kaush Arha akiwakaribisha wadau wanaoshiriki mkutano huo kutoa maoni yao katika udhibiti wa ujangili ulioshika kasi.
Akizungumza kwa niaba ya mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Kenya na Msumbiji alisema Umoja wa Mataifa unajisikia furaha kuona mataifa wanachama yanakabilian na changamoto ya ujangili na uhifadhi wa misitu kwa namna ambavyo itasaidia kizazi kijacho.
Mratibu huyo alisema kwamba ujangili unatishia maendeleo, mazingira na usalama kitu ambacho Umoja wa Mataifa unakipiga vita.
Anasema biashara ya bidhaa za wanyamapori zinahatarisha uwepo wa wanyama ambao tayari wapo katika hatari ya kutoweka, unasababisha rushwa na migogoro ambayo inahatarisha maihsa ya watu.
Alisema kwa sasa dunia imekuwa ikipungukiwa na tembo wa Afrika kwa kasi isiyokubalika kutokana na vitendo vya majangili na hivyo kutaka jamii kushirtikiana kukabiliana na vitendo hivyo.
Mratibu huyo amesema uhalifu unaofanyika kwa wanyamapori na misitu ni lazima ukomeshwe kwa manufaa ya wananchi .
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Tonia Kandiero akizungumza katika mkutano huo.
Alisema Tanzania inastahili kupongezwa kwa kuitisha mkutano wa kujadili ujangili Mei mwaka huu na sasa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kikanda wa kukabiliana na ujangili.
Alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kuimarisha ushirikiano wake na mamlaka mbalimbali zinazoendelea kukabiliana na ujangili na kupotea kwa misitu duniani ili kuhifadhi urithi wa dunia.
Alisema Umoja huo kupitia mashirika yake mbalimbali watawezesha mambo mbalimbali ili kukabiliana na ujangili na uharibifu wa misitu.
Alisema itaendelea kusapoti programu zinazokuza uchumi wa wananchi waliopo karibu na hifadhi za wanyamapori na misitu ili waone umuhimu wa kushiriki kuhifadhi wanyama na misitu husika.
Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mh. Sinikka Antila pamoja na Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke nao ni miongoni mwa wadau wanaohudhuria mkutano huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano),Ummy Mwalimu akishiriki mkutano huo.
Mwenyekiti wa mkutano mkubwa wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori ambaye pia ni Makamu mwenyekiti wa ICCF Group, Dr. Kaush Arha akiteta jambo na mgeni rasmi Waziri wa Mali asili na utalii, Mh. Lazaro Nyalandu.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Bw. Philippe Poinsot (katikati) akimsikiliza mdau kutoka AWF akitoa maoni yake kwenye mkutano huo uliofunguliwa rasmi leo jijini Arusha.
Pichani juu na chini ni washiriki mbalimbali wa mkutano wa kikanda unaozungumzia ujangili na hifadhi endelevu uliofunguliwa rasmi leo jijini Arusha.