Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKOCHA MCHEZO WA WAVU WAPATIWA MAFUNZO ARUSHA

MICHEZO mingi hapa nchini inashindwa kuendelea na kufikia kiwango cha
kimataifa kutokana na kutokuwepo kwa viongozi waadilifu na wanaojitoa
badala yake kufanya michezo kuwa dili.

Hayo yalisemwa  na Mdau wa michezo nchini, Deo Mtui wakati
akifungua semina ya siku sita ya  makocha wa mchezo wa wavu
iliyoandaliwa na Chama cha mpira wa wavu Tanzania(TAVA) inayofanyika
Moshono jijini Arusha.

Alisema kuwa,tatizo lililopo katika timu nyingi za michezo ni
kutokuwepo kwa viongozi waadilifu ambao wamekuwa wakiitumia michezo
kama dili kwa kujipatia fedha ,kitendo ambacho kimechangia idadi kubwa
ya wafadhili kupoteza imani.

Mtui alisema kuwa, endapo nchi ya Tanzania itahitaji kusonga mbele
kimichezo na kuweza kucheza kimataifa ni lazima wawepo kwanza viongozi
wenye mapenzi mema na michezo na waadilifu ambao wataweza kuinua
michezo badala ya kuididimiza .

‘kwa kweli hali hiyo imekuwa ikiwafanya wafadhili wenye nia ya
kusaidia michezo kutoendelea na ufadhili wao kutokana na kuwepo kwa
viongozi ambao wamekuwa wakifanya michezo dili na kujinufaisha kupitia
michezo hiyo na hivyo timu hizo kuendelea kudidimia kila siku bila
mafaniko yoyote’alisema Mtui.

Naye Mwenyekiti cha Chama cha mpira wa wavu Arusha(AVA) ,Rashidi
Mkanga alisema kuwa,mafunzo hayo ni muhimu sana kwa makocha hao ambao
watasaidia kuinua kiwango cha michezo mkoani Arusha.

Alisema kuwa,lengo la mafunzo hayo ni kupata makocha wazuri ambao
watazisaidia timu zao na hatimaye kuweza kupata timu bora ambayo
itachezea mkoa na hatimaye ngazi za juu.

Mkanga alisema kuwa,wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuendesha michezo hiyo ,ukosefu
wa vitendea kazi vifaa vya michezo,na kuwepo kwa upungufu wa wataalamu
wa mchezo huo.

Post a Comment

0 Comments