Muonekano wa daraja la waenda kwa miguu lililopo eneo la Furahisha, mkoani Mwanza. Ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99 na limejengwa na kampuni ya Nyanza Roads Works.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongela (kulia), wakishuka ngazi za daraja la waenda kwa miguu lililojengwa eneo la Furahisha, alipokagua ujenzi wake mkoani Mwanza.
Mhandisi Mkazi anayesimamia uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Mwanza Bw. Geofrey Asulumenye, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, upanuzi wa njia za kurukia ndege katika kiwanja hicho mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mkazi Bw. Geofrey Asulumenye (kulia), kuhusu uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Mwanza, alipokuwa akikagua uwanja huo. Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa Daraja la waenda kwa miguu lililopo eneo la Furahisha na barabara ya kutoka Furahisha hadi Pasiansi yenye urefu wa KM 2.7, imekamilka kwa asilimia 99 Mkoani Mwanza.
Prof. Mbarawa amesema hayo wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujezi wa daraja hilo katika ziara yake ya kikazi mkoani humo na kuridhishwa na ukamilishwaji wa ujenzi wake.
“Daraja hili litaondoa changamoto kwa wananchi wanaotembea kwa miguu na litapunguza au kuondoa adha ya msongamano wanaovuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amewataka wananchi kutunza daraja hilo na miundombinu yake ili liweze kutumika kwa muda mrefu kwani limekuwa nembo ya Mkoa wa Mwanza.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongela, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kujenga Daraja la Furahisha kwa kuwa limebadilisha mandhari ya Jiji hilo.
“Jiji la Mwanza ni kitovu cha Kanda ya Ziwa, wananchi wameguswa moja kwa moja na mradi wa ujenzi wa daraja hili”, amesema Bw. Mongela.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mwanza, Eng. Marwa Rubirya amemweleza Prof. Mbarawa kuwa kazi iliyobaki katika daraja hilo nikuweka taa za urembo.
Ameongeza kuwa Daraja hilo pamoja na barabara yake zimegharimu kiasi cha zaidi ya cha shilingi Bilioni nne na linatarajiwa kuanza kutumika ndani ya siku mbili zijazo.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa amekagua upanuzi wa barabara ya Makongoro hadi Uwanja wa Ndege wenye urefu wa KM 5.3, ambapo malipo ya awali yameshalipwa kwa mkandarasi na mradi unatarajiwa kukamilika mapema kabla ya muda ambao umepangwa mwezi Mei mwakani.
Prof. Mbarawa amekagua uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Mwanza ambao umehusisha ujenzi wa jengo la mizigo, barabara za njia za ndege, jengo maalum la kuongozea ndege (Control Tower) na upanuzi wa urefu wa uwanja hadi kufikia KM 3.8 na kuagiza TANROADS kusimamia uboreshaji wa kiwanja hicho ili kikamilike kwa wakati uliopangwa.
Amesema kuwa hatua inayofuata ni kujenga jengo la kisasa la abiria lenye hadhi ya kimataifa ambalo litachukua na hadhi ya kiwanja hicho.
Uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini ni moja ya mkakati wa Serikali katika kukuza sekta ya usafiri wa anga na kuongeza pato la Taifa.