Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza na viongozi na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo - Kata ya Ubungo alipofanya ziara ya kikazi katika Kata hiyo ili kupokea maoni, ushauri na kusikiliza kero za watumishi wa umma leo Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maji (Water Institute), Dkt. Shija Kazumba akiwasilisha hoja mbalimbali zinazowahusu watumishi wa umma kutoka taasisi anayoiongoza wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo - Kata ya Ubungo kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Afisa TEHAMA wa Ofisi ya Rais-Utumishi, Bw. Dotto Namkaa akiwasilisha mada kuhusu namna ya kujisajili katika Tovuti ya Watumishi (Watumishi Portal) wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo -Kata ya Ubungo kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akifafanua hoja mbalimbali alizopokea kutoka kwa watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo - Kata ya Ubungo (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi na watumishi hao leo Jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Kisare Makori na kushoto kwake ni Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe. Boniface Jacob.
Sehemu ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo - Kata ya Ubungo wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) (Hayupo pichani) wakati wa kikao kazi na watumishi hao kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mamlaka za ajira katika utumishi wa umma nchini zimeelekezwa kufanya marekebisho ya taarifa za watumishi wa umma wanaotarajiwa kustaafu ili waweze kupata stahili zao kwa wakati kama inavyostahili.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo - Kata ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kairuki amesema wapo watumishi wa umma ambao walipandishwa vyeo lakini muda wao wa kustaafu umekaribia na bado hawajafanyiwa mabadiliko yoyote katika taarifa zao.
“Natumia fursa hii kuwaelekeza waajiri wote katika utumishi wa umma warekebishe taarifa za watumishi hawa wanaokaribia kustaafu ili waweze kupata haki na stahili zao,” Mhe. Kairuki amesema serikali inawajali watumishi wa umma na kuongeza wale ambao tayari wameshastaafu, watafutwe na wajaze fomu maalum za madai kupitia kwa waajiri wao ili serikali iwalipe stahili zao kadri inavyostahili.
“Nawaagiza waajiri kupitia kwa Maafisa Utumishi wao, wawatafute ili waweze kujaza fomu maalumu na kuweza kupata haki zao kwani Serikali ipo kwa ajili ya watu wote hivyo hakuna haki ya mtumishi wa umma yeyote itakayopotea,” Mhe. Kairuki amesema.Mhe. Kairuki amewata watumishi wa umma kutimiza wajibu wao kwa weledi ili kuboresha utendaji kazi. “Serikali ni mimi na wewe hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ipasavyo ili kujenga uchumi wa nchi yetu”.
Awali, akimkaribisha Mhe. Kairuki kuzungumza na Watumishi wa Kata ya Ubungo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Kisare Makori amempongeza Mhe. Waziri Kairuki kwa utaratibu anaoufanya wa kukutana na watumishi wa umma kwa kusikiliza maoni pamoja na changamoto wanazozikabili katika utendaji kazi na kuzifanyia kazi.
“Kinachofanyika sasa ni jambo la kipekee sana kwa Waziri Kairuki mwenye majukumu mazito kutoka ofisini kwake na kuja kuzungumza katika kikao kama hiki na watumishi wa umma, kwa niaba ya viongozi wenzangu wa Wilaya ya Ubungo, nampongeza sana,” Mhe. Makori amesema.
Mhe. Makori amewataka watumishi wa umma wa Ubungo kuitendea haki ziara ya Waziri Kairuki kwa kutekeleza maagizo yote yanayotolewa.Mhe. Kairuki yupo katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es salaama ambapo leo ni siku ya saba akiwa katika Kata ya Ubungo kwa kukutana na watumishi wa umma wa kada zote katika vikao kazi.
Lengo la kukutana na watumishi wa umma ni kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini ili kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS-UTUMISHI