Wakuu
wa vituo vidogo, Wakaguzi wa Tarafa pamoja na Polisi kata wameambiwa
kwamba wanatakiwa kuwa karibu na wananchi hasa kwa kushiriki shughuli za
kijamii kama vile misiba na matatizo mbalimbali hali ambayo itasaidia
kupata taarifa nyingi za uhalifu.
Akizungumza
katika kikao hicho kilichowahusisha pia watendaji wa kata mbalimbali za
halmashauri ya jiji la Arusha kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika
ukumbi wa bwalo la Polisi lililopo mjini hapa, kamanda wa polisi mkoa wa
Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kutatua matatizo ya
kihalifu yanayowakabili wananchi si njia pekee ya kuwa karibu na
wananchi bali pia askari hao wanatakiwa kushiriki kwa namna moja au
nyingine katika shughuli za kijamii katika maeneo yao.
Alisema
kitendo hicho cha askari hao kuishi vizuri na wananchi nje ya kazi yao
ya Upolisi kitasabaisha wananchi wajione wapo karibu na askari kwa kila
jambo hali ambayo itasaidia kupata taarifa zaidi za kihalifu ambazo
hatimaye watazifanyia kazi.
”Ushirikiano
wenu pia ujikite kushiriki katika masuala ya kijamii kama vile misiba,
lakini pia kuna matatizo mengine kama ya kukatika kwa umeme Polisi kata
unapaswa uwasiliane na Tanesco ili kujua tatizo lipo wapi na kisha
kuwajulisha wananchi wa kata yako”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Aidha
Kamanda Mkumbo alisisitiza kudumishwa kwa ushirikiano baina ya askari
hao na viongozi wa mitaa pamoja na kata ili kujenga umoja imara
utakaosaidia katika kupambana na uhalifu na kuwaeleza watendaji nao
wanatakiwa kuwaambia mabalozi wawe na madaftari la usajili wa wageni
katika maeneo yao yatayowawezesha kujua tarehe ya kuingia na kuondoka
hali ambayo itasaidia kuimarisha usalama.
Kwa
upande wake Afisa Mtendaji wa kata ya Ngarenaro Bw. Brayson Nassari
aliendelea kuhimiza ushirikiano katika utendaji wa kazi baina ya Polisi
kata na watendaji hali ambayo itasaidia kuimarisha utulivu na amani
ndani ya jiji la Arusha.
Naye
Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi (SSP) Emmanuel Tille
alizidi kuwasisitiza Polisi kata wawe na vikao vya mara kwa mara na
wananchi hali itakayowasaidia kutoa elimu ya ulinzi shirikishi na kupata
taarifa lakini pia aliwaeleza watendaji wa kata waendelee kutoa taarifa
na kufichua sehemu zenye viashiria vya uhalifu ili zifanyiwe kazi kwa
haraka.
Kuwepo
kwa mahusiano ya karibu baina ya Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha na
wananchi kumesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya uhalifu
ambapo takwimu za hivi karibu zilizotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa
Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo zinaonyesha kwamba kwa
kipindi cha miezi sita toka Januari hadi Juni mwaka huu 2017 uhalifu
umepungua kwa 24.4% ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana 2016.