Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hakuna kijiji nchini kitakachoachwa bila
ya kuunganishiwa umeme katika awamu ya tatu ya mradi unaotekelezwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Amesema
Serikali imetenga Sh1 trilioni kwa ajili ya kusambaza umeme katika
vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa na nishati hiyo.
Waziri Mkuu amesema hayo alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wilayani Ruangwa.
Amesema
hayo katika mikutano aliyoifanya kwenye vijiji vya Chiapi, Nandanga,
Mbecha na Luchelegwa, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya
siku nne mkoani Lindi.
“Rais
John Magufuli anajali wananchi, hivyo ametenga fedha nyingi
zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo vya
Wilaya ya Ruangwa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni Sh27,000 tu,”
amesema katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.
Amesema
wananchi hawatawajibika kulipia nguzo na fomu za maombi ya
kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimebebwa na
Serikali.
Amesema
lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na
kwa vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa,
vitafungiwa umeme jua (sola) hivyo kufungua fursa za ajira na kukuza
uchumi.
Waziri
Mkuu amesema huduma hiyo ni muhimu kwa kuwa mbali ya kutumiwa majumbani
lakini pia kwa kusogezwa karibu na maeneo ya pembezoni itawezesha
zahanati, shule, viwanda na vituo vya afya kuwa na umeme.
Meneja
wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Lindi, Johnson Mwigune
amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu mkandarasi aliyepangwa
kufanya kazi katika vijiji hivyo atakuwa ameanza kusambaza umeme.