Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF) limewavua uanachama
wabunge wanane wa chama hicho kwa madai ya utovu wa nidhamu ikiwa ni
pamoja na kukisaliti chama hicho.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya CUF,
Buguruni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema, mbali na wabunge hao, baraza hilo pia limewavua
uanachama madiwani wawili wa viti maalumu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa
makosa kama hayo.
Lipumba
amesema wabunge hao waliovuliwa uanachama ni miongoni mwa wabunge kumi
waliosusia wito wa kwenda kujieleza juu ya tuhuma zinazowakabili za kula
njama na CHADEMA ili kuweza kumuondoa yeye madarakani.
Aidha,
Lipumba aliwaambia waandishi wa habari kuwa, taarifa kuhusu uamuzi huo
tayari zimeshatumwa kwenda kwenye Ofisi ya Spika wa Bunge na Msajili wa
Vyama vya Siasa kwa ajili ya hatua zaidi.
Wabunge 10 walioitwa kuhojiwa na chama hicho inadaiwa kuwa ni wale wanaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif.
Baadhi
ya wenyeviti wa serikali za mitaa zilizopo chini ya CUF, wamesema
binafsi hawatokuwa tayari kuhojiwa kwani hawamtambui kiongozi huyo.