MBUNGE JUMAA HAMIDU AWESSO AFANIKISHA NDOTO ZA VIJANA PANGANI



 Mbunge wa Pangani Jumaa Hamidu Awesso aliyevaa shati la bluu akiwa na baadhi ya viongozi wa simba mapema leo wakati alipowatembelea vijana wake wanaofanyiwa majaribio na klabu hiyo
 Kijana Abdallah Hamisi Abeid  maarufu kam Jr kutokea Pangani aliyechaguliwa kujiunga na klabu ya Simba B
Kijana Abdallah Hamisi Abeid akiwa na wenzake waliofanyiwa majaribio na Simba B 
 Na Mohammed Hammie

Mbunge wa jimbo la Pangani Jumaa Hamidu Awesso hatimae amefanikisha ndoto za kijana Abdallah Hamisi Abeid  maarufu kama Jr kutokea Pangani Mjini kwa kuchaguliwa kuchezea klabu ya Simba B baada ya kupenya katika mchujo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Mheshimiwa Awesso amesema kuwa, kufanikiwa kwa kijana huyo ndio mwanzo wa kuibua vijana wengine wenye vipaji vya soka katika jimbo lake la Pangani.

Awali mbunge huyo kijana aliandaa vijana wanne kwa ajili kuwapeleka kwenye klabu hiyo kongwe kwa ajili ya kufanyiwa majaribio, kwa lengo la kufanikisha ndoto zao za kuchezea klabu kubwa hapa nchini.

"Nilichukua vijana wanne na kuwaleta hapa Dar es salaam kwenye klabu ya Simba ambao ni Abdallah Hamisi aliyepata nafasi, wengine ni Bakari Mohammed, Gasper Anthony na Sueli Salum ambao kwa sasa naendelea kuwafanyia mpango wa kufanya majaribio kwenye klabu nyengine" amesema Mheshimiwa Awesso.

Kijana Abdallah Hamisi au Jr ambaye wengi humfananisha na Mbwana Samatta, anatokea katika klabu ya Blackburn ya Pangani Mjini ambayo imekuwa na mashabiki wengi kutokana na kujaa vijana wengi wenye vipaji vya kusukuma kabumbu.

"Kabla sijajiunga na Black Burn nilitokea klabu nyengine ya Pangani United, kwa hiyo sina uzoefu mkubwa sana lakini nina uwezo wa kipekee na ndio maana nimechaguliwa kujiunga na Simba B" anasema Jr.

"Pia namshukuru sana Mbunge wangu Jumaa Awesso kwa jitihada zake za kutukusanya sisi vijana wenye vipaji na kuhakikisha tunafikia ndoto zake, kwa kweli ni mbunge pekee ambaye anaonyesha mapenzi ya dhati kwa wananchi wake, sio tu katika soka hata katika mambo mengine ya kimaendeleo" amesema Jr.

Jr amewataka pia vijana wengine wilayani Pangani na Tanzania kwa ujumla kuwa na uthubutu na kujiamini pindi wanapopatiwa fursa ya kuonyesha vipaji vyao mahala ambapo pana uwezekano wa kutoka kimaisha.

Pia amewataka vijana wenzake ambao hawakupata nafasi hiyo, kutokata tamaa na badala yake waendelee kufanya majaribio kwenye vilabu vyengine vikubwa hapa nchini.

Mbunge Jumaa Awesso ameahidi kuendelea kuibua vijana wengine wenye vipaji kutokea Pangani pasipo kujali itikadi, ili vijana hao wawe chachu ya kuitangaza wilaya hiyo na kuiletea heshima hata ikibidi katika anga za kimataifa.
Mohammed Hammie Rajab
PR Manager/Radio Editor
Uzikwasa/Pangani Fm Radio
P.o Box 1, Pangani
E-mail: ankomo25@yahoo.com
Phone: +255678900424
              +255719000010  

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post