Na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Watu wanne ambao bado hawajafahamika
wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 35 wanaosadikiwa kuwa
ni majambazi wameuawa baada ya kupigwa risasi na askari Polisi. Tukio hilo
lilitokea jana tarehe 21.02.2014 muda wa saa 1:00 jioni katika bar moja iitwayo
Pama iliyopo maeneo ya Makao Mapya jijini hapa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Liberatus Sabas alisema kwamba, tukio hilo lilitokea mara baada ya jeshi la
polisi Mkoani hapa kupata taarifa toka kwa raia wema kwamba watu hao walikuwa
wanapanga kwenda kufanya tukio la uhalifu katika kituo kimojawapo cha kuuzia
mafuta kilichopo jijini hapa ambapo ufuatiliaji wa taarifa hiyo ulianza.
Ilipofika muda huo askari hao
walikwenda katika bar hiyo na mara baada ya majambazi hao kuwaona askari hao
walihisi wanafuatiliwa ndipo mmojawao ghafla alitoa bastola na kufyatua risasi tatu ambapo moja
ilimparaza askari mmoja aitwaye F. 1416 D/Ssgt Richard katika mkono wake wa
kushoto
“Kufuatia hali hiyo askari nao waliamua kujibu
mapigo kwa kupiga risasi ambapo wanne kati ya watano walijeruhiwa na mmojawao alifanikiwa
kukimbia akiwa na silaha inayosadikiwa kuwa ni SMG”. Alisema Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas alisema kwamba,
majambazi hao walifariki dunia wakiwa njiani kuelekea hospitali ya Mount Meru
kwa ajili ya matibabu na miili yao imehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya
utambuzi toka kwa ndugu na jamaa wa karibu.
Aidha Kamanda Sabas alisema, katika
eneo la tukio askari hao walipata bastola moja aina ya Star yenye namba 42640
FNH PISTOLE MODEL KAL 7.65 ikiwa na risasi tatu katika magazine, maganda matatu
ya risasi pamoja na begi moja dogo la mgongoni lenye rangi nyekundu likiwa na
risasi nne hivyo kufanya jumla ya risasi saba kupatikana.
Bado Jeshi la Polisi Mkoani hapa
linaendelea na upelelezi kuhusiana na tukio hilo ikiwa ni pamoja na kumtafuta
mtuhumiwa mmoja aliyekimbia.
Kufuatia tukio hilo Kamanda Sabas
aliendelea kuwashukuru wananchi wa Arusha kwa ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa
kwa jeshi la Polisi Mkoani hapa na kuwasihi waendelee kutoa taarifa za uhalifu
na wahalifu hali itakayosaidia kukomesha matukio ya uhalifu mkoani hapa.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia