KAMPUNI ya Atomtek Nuclear Energy ya Uturuki inatarajia kutumia
dola milioni 10 za Marekani kwa ajili ya kuimarisha ulinzi maeneo ya
bandarini, viwanja vya ndege na barabarani ili kuhakikisha mali
zinazosafirishwa zinakuwa salama.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Habari wa kampuni hiyo, Yusufu Mjema,
alipokuwa akitoa taarifa ya kampuni hiyo mjini Arusha, ambayo imeomba
serikali kuwekeza hapa nchini ili kuimarisha ulinzi kwa kuongeza vifaa
kwenye maeneo husika ili kudhibiti uingizaji wa bidhaa zisizo salama.
Mjema alisema endapo kampuni hiyo itapewa kibali cha kuanza uwekezaji
hapa nchini katika awamu ya kwanza itatumia kiasi hicho cha fedha na
kwamba itaendelea kutumia dola milioni 80 za Marekani ambapo itaweka
mitambo ya magari 400 bandarini na helikopta.
Alisisitiza kuwa endapo kampuni hiyo itakubaliwa, itasaidia kutokana
na vifaa vilivyopo sasa kutokidhi mahitaji katika maeneo husika na
itaweza kuona mali ambayo si salama inayosafirishwa kwa njia ya meli
mita 300 kabla ya kutia nanga na kwa upande wa ndege futi 1,800 kutoka
angani huku magari yakifanya doria katika maeneo mbalimbali.
“Kampuni hii ya Uturuki inaomba kuwekeza hapa nchini ili kusaidia
serikali kuimarisha ulinzi na kuhakikisha bidhaa zote zinazosafirishwa
kwa njia zote ni salama na endapo maombi yatapitishwa itaanza kazi
Julai mwaka huu,” alisema.
Kwa upande wake Dennis Mwalongo ambaye ni mwanasayansi katika Tume ya
Taifa ya Nguvu za Atomu mkoani Arusha alisema tume hiyo inafanya kazi
ya kuhakiki vifaa vinavyotumika katika sehemu za mionzi ili kuona iwapo
imezidi na kutoa ushauri kwa wafanyakazi.
Alisema wagonjwa wanaotibiwa kwa njia ya mionzi wanapata tiba sahihi,
tume hiyo pia hupima kiwango cha mionzi kwa wafanyakazi wa sehemu za
mionzi na kuwashauri kama kiwango kipo juu ili kuepusha hatari ya
kupata saratani.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ibrahim Kuzu na wafanyakazi wengine
wamefanya ziara ya siku moja katika tume ya Atomu Arusha kuangalia
namna vyakula na vitu vingine vinavyopimwa kwenye maabara na kutambua
elementi zilizopo iwapo zipo juu ya kiwango na kushauri kutotumika kwa
bidhaa husika.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia