BREAKING NEWS

Friday, February 21, 2014

WAPENDEKEZA KURA ZA SIRI KWENYE BUNGE LA KATIBA


Rasimu za kanuni za uendeshaji Bunge Maalumu la Katiba zimependekeza kutumika kwa utaratibu wa kupiga kura ya siri wakati wa kupata uamuzi wa kupitisha Rasimu ya Katiba.
Endapo mapendekezo hayo yatapitishwa, hoja ya Katiba Mpya itakayowasilishwa na Kamati ya Bunge Maalumu la Katiba, itaamuliwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na idadi kama hiyo ya wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar.

Upigaji kura huo kwa siri, umepongezwa na baadhi ya wabunge kwa maelezo kuwa utatoa fursa kwa wajumbe kupiga kura hizo kwa uhuru na bila kushinikizwa na misimamo ya vyama au taasisi zilizowapendekeza.

Kanuni hizo zimekuja wakati CCM, kikiwa kimewaagiza wajumbe wake ambao ndiyo wengi bungeni, kutetea muundo wa Serikali mbili badala ya ule wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Pamoja na CCM kuweka msimamo wa kuwataka wajumbe wake kuutetea mfumo huo, kumeibuka mgawanyiko mkubwa huku baadhi yao wakitarajiwa kukitosa na kuunga mkono mfumo wa Serikali tatu.

Kanuni ya 82(1) ya rasimu hiyo, imeweka bayana kuwa utaratibu utakaotumika kupata uamuzi baada ya mwenyekiti kulihoji Bunge ni wa ama kura ya siri au ya kielektroniki.

“Wakati wa kupiga kura ya siri, kila mjumbe atapiga kura ya Ndiyo au Hapana kwa kutumia karatasi za kupigia kura zitakazokuwa zimeandaliwa na Katibu wa Bunge,” inasomeka kanuni ya 83(1).

Kanuni hiyo imeweka wazi kuwa kupiga kura kwa mujibu wa masharti ya kanuni hiyo, itakuwa ni wajibu na haki ya msingi ya kila mjumbe na kwamba kila mjumbe atapiga kura kwa binafsi yake.

Hatua ya wajumbe kupiga kura hiyo, itatanguliwa na kazi ya kila Kamati ya Bunge Maalumu, kujadili rasimu ya katiba hiyo kulingana na mgawanyo wa majukumu. Kamati 17 zitashughulikia ibara za rasimu.

Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ataagiza taarifa ya kamati iwekwe kwenye orodha ya shughuli kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni kwa mjadala.

Kanuni hizo zimeeleza kuwa wakati wa mjadala huo, mjumbe yeyote anaweza kushauri na kutoa mapendekezo ya marekebisho au mabadiliko kwa ajili ya kuboresha sura ya rasimu inayohusika.

Hata hivyo, Kanuni za 78 (11) na 78 (12) za rasimu hiyo, zinapendekeza mwenyekiti asiruhusu hoja yoyote inayokiuka sheria au pendekezo la kamati linalohusu jambo lililo nje ya mamlaka ya Bunge.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates