Trafiki wala rushwa sasa kusota njaa
Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani nchini, kina mpango wa kuanzisha utaratibu mpya wa kulipa faini zote za makosa ya barabarani kupitia benki na mitandao ya simu za mkononi.
Utaratibu huo unalenga katika kupunguza malalamiko
ya wananchi kuhusu vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya askari
wa usalama barabarani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga,
alisema utaratibu huo unatarajiwa kuanza wakati wowote ndani ya mwaka
huu baada ya makao makuu ya jeshi hilo, kuuidhinisha.
Alisema kwa sasa jeshi hilo lipo katika mchakato wa kuhakikisha kuwa utaratibu huo unaanza mapema.
Alisema chini ya mfumo huo, mlipaji atapewa risiti ya benki au mtandao wa simu ambao malipo hayo yatapitia.
“Muda wowote ndani ya mwaka huu utaratibu mpya
utaanza, tunataka kuboresha mfumo wa ulipaji faini na kuondokana na
mianya ya rushwa inayofanywa na baadhi ya askari wa usalama wa
barabarani kama inavyolalamikiwa na wananchi” alisema Kamanda Mpinga.
Alisema licha ya mfumo huo kuwa mpya viwango vya faini zitakazotozwa havitabadilishwa wala kuongezwa.
Kuhusu askari wa kikosi hicho wenye vitabu bandia
vya faini kuwa sababu ya kubadilisha utaratibu wa sasa, Kamanda Mpinga
alisema ofisi yake haijapata taarifa za uhakika wala ushahidi kuhusu
vitabu hivyo.
“Tatizo hili linazungumzwa hakuna taarifa kamili
za kupatikana kwa vitabu feki lakini vitabu hivyo vinaweza kuwepo na
vikatumika kinyume na sheria ndiyo maana tutaanzisha utaratibu huu,”
alisema kamanda.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia