Tanzania itapata nini kwa kuihujumu Rwanda?
Serikali mwishoni mwa wiki ililazimika kukanusha vikali habari iliyochapishwa na gazeti la Serikali ya Rwanda kwamba Rais Jakaya Kikwete anavisaidia vikundi vya waasi nchini humo kuihujumu Serikali ya Rais Paul Kagame.
Pasipo kuthibitisha au kuonyesha vyanzo vya tuhuma
hizo ambazo Serikali ya Tanzania imesema hazina msingi wowote, Gazeti
hilo la ‘The News of Rwanda’ limeonyesha wazi kwamba, huenda limebeba
ajenda ya siri inayosukumwa na baadhi ya wanasiasa nchini humo ya
kuharibu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Tamko la Serikali kupitia kwa Kaimu Balozi wa
Tanzania nchini Rwanda, Francis Mwaipaja limesema Rais Kikwete
amesikitishwa na habari hizo za uongo na kusema zinaweza kujenga chuki
na kuwachanganya wananchi wa nchi hizo jirani na rafiki.
Jambo ambalo tunadhani Serikali ya Tanzania
itahitaji ufafanuzi kutoka Kigali ni msimamo wa Serikali ya Rwanda
kuhusu tuhuma hizo zilizochapishwa na gazeti hilo inalolimiliki. Itakuwa
vigumu kwa Serikali kujenga hoja kwamba gazeti lake lilichapisha tuhuma
hizo nzito pasipo serikali yenyewe kujua na pengine kuridhia.
Tunaposema hivyo hatuna maana kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa imara siku zote.
Mwaka uliopita uhusiano kati ya viongozi wa nchi
hizo mbili ulidorora baada ya Rais Kikwete kumshauri Rais Kagame kufanya
mazungumzo na vikundi vya waasi vya FDLR na RNC ili kupata maridhiano,
lakini Rais huyo aliuchukulia ushauri huo kama matusi kwa nchi yake na
kusema hawezi kukaa pamoja na watu aliodai walifanya mauaji ya kimbari
ya mwaka 1994 ambapo watu zaidi ya 800,000 waliuawa.
Vilevile, kitendo cha majeshi ya ulinzi ya
Tanzania mwaka jana kushiriki kupambana na kukisambaratisha kikundi
kilichokuwa kikihusishwa na Serikali ya Rwanda cha M23, ambacho kilikuwa
kikiendesha hujuma dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC), kilimkasirisha sana Rais Kagame.
Hali hiyo ilisababisha Kenya, Uganda na Rwanda
kuitenga Tanzania katika baadhi ya mambo muhimu katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC).
Hata hivyo, wakati juhudi za kurejesha uhusiano
baina ya nchi hizo mbili zikionekana kuzaa matunda, ndipo gazeti hilo
lilipoibuka na habari hizo za kutunga dhidi ya Rais Kikwete na serikali
yake kwa lengo la kuweka mazingira magumu ili kukwaza juhudi hizo.
Kama tulivyosema hapo juu, wapo watu wanaofaidika
inapokuwapo hali ya kutoelewana baina ya viongozi wa nchi hizo jirani na
rafiki.
Tunasema hivyo, kwa sababu inawezekanaje gazeti
limtuhumu Rais Kikwete kwamba katika nyakati tofauti mjini Dodoma na
Ikulu jijini Dar es Salaam alikutana na Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda,
Faustine Twagiramungu pamoja na viongozi wa RNC na makamanda wa FDLR,
wakati dunia nzima inajua kwamba wakati huo alikuwa Davos, Uswisi
akihudhuria Mkutano wa Dunia Kuhusu Uchumi (WEF), ambapo alikutana na
viongozi mbalimbali duniani, wakiwamo Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza,
Niuck Clegg na Mkuu wa USAID, Rajiv Shah.
Tunashangazwa pia na madai ya gazeti hilo eti
Tanzania imeanzisha taasisi ya kuwasaidia waasi wa Rwanda na ilitoa pasi
za kusafiria kwa viongozi wa makundi ya waasi yaliyotajwa hapo juu.
Tunaishauri Serikali kuchunguza chanzo cha tuhuma hizi za kuchonga. Hivi
Tanzania itapata nini kwa kuihujumu nchi kama Rwanda?
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia