WAFANYA BIASHARA WA MKOANI MANYARA WATESEKA KWA KUKOSA OFISI YA TRA MKOANI KWAO
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Manyara, imeiagiza Mamlaka ya mapato
nchini (TRA) mkoani humo, kufungua ofisi kwenye Wilaya za Simanjiro na Hanang’ ili
kuwawezesha wafanyabiashara walipie ushuru na kodi wakiwa eneo la karibu.
Imeelezwa kuwa, wafanyabiashara wa wilaya za Simanjiro na Hanang’
wanakabiliwa na tatizo la kutokuwa na ofisi za kulipia mapato yao, hivyo kulipia
kwenye ofisi za TRA za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na wilayani Mbulu.
Akizungumza kwenye mkutano wa 20 wa kamati hiyo mjini Babati juzi,
mkuu wa mkoa huo, Elaston Mbwilo alisema ofisi hizo zinatakiwa kufunguliwa
kwenye miji ya Mirerani wilayani Simanjiro na Katesh wilayani Hanang.’
Mbwilo alisema maeneo hayo yanatakiwa kuwa na ofizi za TRA ili
kukusanya mapato yatakayowezesha mkoa huo kuingia mapato nchini, kuliko hivi
sasa kwani baadhi ya wafanyabiashara wanalipia nje ya mkoa wake.
Alisema mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hanang, Felix
Mabula aliahidi kutoa chumba kwenye jengo la hamashauri tangu Julai mwaka jana,
wakati TRA wanajipanga na utaratibu wa kupata ofisi za kudumu.
“Pia kwenye wilaya ya Simanjiro nao tuliwashauri kutafuta eneo la
muda ili kuongeza mapato kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wake wanalipa kodi
mkoani Arusha na Kilimanjaro,” alisema Mbwilo.
Kutokana na hali hiyo waliazimia Katibu Tawala wa mkoa aandike
barua kwa Kamishna wa TRA kuomba kufunguliwa ofisi kwenye wilaya hizo na
kueleza nanma wanavyopoteza mapato kutokana na kukosa ofisi katika maneo hayo.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wa miji ya Mirerani na
Katesh, walilalamikia ukosefu wa ofisi, kwani watumishi wa TRA huwa wanawavamia
na kutaka mapato hivyo wangekuwa na ofisi wangetoa ushirikiano mkubwa.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia