Viongozi CCM wazidi kuvurugana urais mwaka 2015
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, amewaonya wanachama wa chama hicho wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao akiwataka kuzingatia kanuni za chama hicho, vinginevyo watahukumiwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msekwa alisema
watu hao watahukumiwa na chama akieleza kwamba kutangaza nia kabla ya
wakati ni kukiuka kanuni za CCM, zinazoeleza wazi kuwa wagombea wa
nafasi mbalimbali, watajitangaza baada ya chama kutoa ratiba yake.
Wakati Msekwa akieleza hayo, Mwenyekiti wa Umoja
wa Vijana wa CCM (UVCCM) Sadifa Juma Khamis amesema kuwa kutangaza nia
ya kugombea nafasi yoyoye ndani ya chama hicho siyo dhambi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis
Mgeja ameshambulia Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho John
Malecela aliyetaka CCM imchukulie hatua Waziri Mkuu wa zamani Edward
Lowassa kwa madai ya kuanza mapema kampeni za kusaka urais wa mwaka
2015, hatua inayotafsiriwa kuwa ni kuzidi kuvurugana kwa chama hicho.
Msekwa alisema kuwa CCM inaongozwa kwa mujibu wa
kanuni na Katiba yake na kwamba katika jambo hilo linaloibuka sasa,
kanuni ndiyo zinazohusika zikielekeza wazi mgombea afanye nini na kwa
wakati gani.
“Mimi mwenyewe nilishiriki kuandika kanuni hizo,
utakapofika wakati chama kitatoa ratiba yake na kila mwenye nia atakuwa
na uhuru wa kueleza nia yake. Lakini kutangaza kugombea sasa kabla ya
wakati, ni kukiuka kanuni za CCM na ni kosa kubwa,” alisema Msekwa.
Aliwataka wanaCCM wote kuepuka kukiuka kanuni za
chama hicho akisisitiza kuwa wote watakaohusika kuzivunja, wataadhibiwa
kwa mujibu wa Kanuni na Katiba ya chama hicho.
Alisema kuwa wanaodhani kwa kufanya hivyo
wanakivuruga chama, wanafanya makosa kwani watakaoathirika ni wale
wanaovunja kanuni zilizowekwa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Chama
Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis alionyesha kupingana na maneno
hayo ya Msekwa, huku yeye akisema kutangaza nia ya kugombea nafasi
yoyote ndani ya chama siyo kosa, mradi mhusika awe na nia, sifa na
uwezo.
Alisema kuwa ingawa UVCCM haijakaa kujadili watu
hao, lakini haoni kosa lolote kwa mwanaCCM kujitokeza na kutangaza nia
yake hadharani.Wakati huo huo, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi
katika Umoja wa Vijana (UVCCM), Paul Makonda ametakiwa kuwaomba radhi
viongozi wa dini kutokana na kauli yake ya hivi karibuni kuwa masheikh
na maaskofu wakiwemo vijana wanaotaka fedha za bure waende kwa Edward
Lowassa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Mwenyekliti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamisi Mgeja alisema
licha ya Makonda kuomba radhi, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), utoe
tamko kueleza iwapo kauli hiyo ni ya Makonda au ndiyo msimamo wa Jumuia.
“Nataka mwenyekiti wa UVCCM Taifa kutoa tamko kuhusu kauli hiyo na pia
viongozi wa dini waombwe radhi kwani walichofanyiwa ni udhalilishaji,”
alisema Mgeja.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia