Na Kitengo cha Mawasiliano - Wizara ya Ardhi
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mhe. William Lukuvi amewapatia hati miliki za Ardhi kwa jamii ya wa
Hadzabe wanaoishi wilayani Karatu Mkoani Arusha.
Waziri Lukuvi amefika katika maeneo yao na kuwapa
hati miliki za kimila kwa vijiji na wanayoishi jamii ya wa Hadzabe na
jamii nyingine za kifugaji ili kulinda maeneo yao ya malisho na maeneo
wanayotumia kuwinda wanyama.
Jamii ya wa Hadzabe ni watu ambao huishi kwa
mfumo wa maisha ya kuwinda, kufuga wanyama pori na kula mimea na matunda
ya miti inayowazunguka. Jamii hii kwa miaka mingi imekuwa ikiishi bila
kufuata mipaka ya maeneo yao na hivyo kusababisha migogoro ya ardhi kwa
jamii nyingine zinazoishi karibu na maeneo yao.
Pamoja na ziara hiyo Mhe. William Lukuvi amtatua
migogoro ya Ardhi ya wananchi wa wilayani Karatu Mkoani Arusha na
wananchi walio na kero za migogoro ya ardhi na kuzipatia ufumbuzi pamoja
na kupokea vielelezo vya kero za wananchi walizoziwasilisha kwa Waziri
ili azitolee maamuzi.
Wananchi wa vijiji vya Mang’ola juu na Midabini
wilayani Karatu Mkoani Arusha walisimamisha msafara wa Mhe. Lukuvi ili
awasikilize kero zao za ardhi, ambapo Waziri Lukuvi alisimama na
kuzitatua pamoja na kumuagiza Mkuu wa wilaya ya karatu Bibi Therezia
Mahongo kutafutia ufumbuzi baadhi ya migogoro hiyo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mhe. William Lukuvi anaendelea na Ziara zake za utatuzi wa Migogoro ya
Ardhi nchini, ambayo imejikita zaidi katika kutatua migogoro ya ardhi ya
Mikoa ya kanda ya Magharibi, Kaskazini na ile ya Kanda ya Ziwa hapa
nchini.
Hadi sasa Mhe. Lukuvi ndani ya mwezi huu wa
Desemba ameishatatua migogoro ya ardhi ya Mkoa wa Kigoma na wilaya zake
za Kigoma mjini, Kasulu na Kibondo na katika Mkoa wa Shinyanga na wilaya
zake za Kishapu na Shinyanga mjini na katika mkoa wa Geita amefanya
ziara katika wilayani Chato.
Pia Mhe. Lukuvi ametatua migogoro ya ardhi ya
Mkoa wa Mara katika wilaya za Musoma na Bunda ambapo kwa Arusha ametatua
migogoro ya wilaya ya Arumeru na Karatu.